Habari Mseto

Askofu Kimengich amshauri Ruto kupunguza makali yake kwa mahakama

January 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

VIONGOZI wa kidini wamemtaka Rais William Ruto kusitisha vita kati yake na Idara ya Mahakama, wakisema malumbano hayo huenda yakaathiri mahakama kuhudumia Wakenya.

Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Eldoret, Dominic Kimengich anazitaka asasi husika zote mbili; afisi ya rais na mahakama, kuacha kuhujumiana na badala yake zifuate taratibu zinazofaa kisheria kushughulikia masuala yanasababisha tofauti baina yao.

Askofu Kimengich alihimiza idara ya mahakama kuhudumia Wakenya kwa njia halali kwa kuzingatia utawala wa sheria na uadilifu.

Akizungumza katika kanisa la Eldoret Sacred Heart, wakati wa kutawazwa kwa zaidi ya mashemasi 80, Askofu Kimengich aliitaka mahakama kushughulikia malalamishi ya ufisadi yaliyoibuliwa na Rais William Ruto ili kuaminika na Wakenya.

“Rais ameibua wasiwasi kuhusu tuhuma za rushwa katika mahakama na jambo la heshima ambalo mahakama inapaswa kufanya; ni kushughulikia masuala hayo na kuhakikisha kwamba wanatoa maamuzi na hukumu zao kwa njia ya haki badala ya kujitetea kupitia vyombo vya habari,” alisema Askofu Kimengich.

Alisikitika kwamba ugomvi kati ya taasisi hizo mbili ni tishio kwa uwiano wa kitaifa na maendeleo kwa ujumla.

Askofu huyo aidha alisikitika kwamba maslahi ya wananchi hayatiliwi maanani na idara hizo.

“Tuko katika hali ambayo maslahi ya nchi sio jambo la kwanza. Mahakama itekeleze majukumu yake kwa kufuata haki na kuongozwa na ukweli, serikali nayo iheshimu maamuzi yanayotolewa na mahakama. Hebu kuwe na heshima kati ya mihimili hii miwili ya serikali,” aliongeza Askofu Kimengich.

Kwa upande wake Baraza la Maimamu na wahubiri wa Kenya, walishutumu asasi hizo mbili za serikali kwa kuyumbisha maisha ya Wakenya kupitia mvutano baina yao.

Mwenyekiti wa CIPK North Rift Sheikh Abubakar Bini alisema vita kati ya afisi ya rais na mahakama, ni hatari kwa Wakenya ambao wanazitegemea kwa hali na mali.

“Ugomvi huu unatishia ustawi wa Wakenya wa matabaka ya chini, chambilecho msemo kuwa wapiganapo fahali nyasi ndio huumia,” alisema Sheikh Bini.