Serikali yaahirisha uzinduzi wa mtaala mpya, 8-4-4 kuzidi kutumika
Na SAMUEL OWINO
SERIKALI imeahirisha mpango wa kuzindua mtaala mpya wa masomo mwaka ujao ili kutoa nafasi ya kuweka miundo msingi na mashauriano zaidi na washikadau, Waziri wa Elimu Amina Mohamed amesema.
Alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Elimu Jumanne, Waziri Mohamed alisema wizara yake pia ilifikia uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa walimu kupewa mafunzo kuhusu mtaala huo ambao ulitarajiwa kutekelezwa chini ya mfumo mpya wa elimu wa 2-6-6-3.
“Vile vile, tunataka kuhakikisha kuwa walimu wamepewa mafunzo ipasavyo kuhusu yale ambayo wanatarajiwa kutekeleza chini ya mtaala huo. Kufikia saa walimu 79,000 katika maeneo 1,168 wamepokea mafunzo, na idadi hii haitoshi,” Bi Mohamed alieleza.
“Kwa hivyo, ninaweza kuwaeleza kuwa hatuko tayari kuzindua mtaala huo kote nchini. Vile vile, tunapanga kuhakikisha kuwa mtaala huo unaanzishwa katika vyuo vya mafunzo ya walimu ili wale watakaohitimu watakuwa tayari kwa utekelezaji wake,” alisema Dkt Mohamed.
“Je, mpango huo uliharakishwa? Na je, ukaguzi wa kindani ulifanywa kuhusu utekelezaji wa mtaala huo mpya?” Seneta wa Nyamira, Okong’o Omogeni, ambaye alionekana kushangazwa na kuahirishwa kwa mpango huo, alimuuliza waziri.
Waziri Mohamed akajibu: “Muundo wa mtaala huo mpya ni mzuri lakini changamoto iko katika utekelezaji wake. Ikiwa utatekelezwa vizuri utawafaidi watoto wetu pakubwa kimaarifa,”
“Nilipoingia katika wizara hii niliangalia mtaala huo mpya na nikaridhika kuwa wale ambao waliutunga walifanya kazi nzuri,” Waziri akawaambia maseneta hao.
Alikuwa ameandamana na Katibu wa Wizara hiyo, Dkt Belio Kipsang na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) Julius Jwan.
Dkt Kipsang aliiambia Kamati hiyo inayoongozwa n Seneta wa Uasin Gishu, Prof Margaret Kamar kwamba wanafunzi ambao walikuwa wakifanyiwa majaribio ya mtaala huo watapandishwa ngazi hadi madarasa ya juu ambapo watafunzwa kwa kutumia mtaala wa mfumo wa elimu wa 8-4-4.
Bw Kipsang alilalamika kuwa sekta ya elimu wakati huu inakabiliwa na changamoto nyingi haswa uhaba wa walimu.