Gavana Nassir atoa basari kwa wanafunzi wote wa kutwa Mombasa kufuatia malalamishi
GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Nassir ametoa basari kwa wanafunzi wote wa shule za kutwa katika kaunti hiyo, ili kupunguza malalamishi yaliyoibuliwa hapo awali ya ubaguzi.
Gavana huyo alisema wanafunzi takriban 33,000 watapokea Sh5,000 ili kuwafaa kujiendeleza kimasomo.
“Kumekuwa na malalamishi kuhusu jinsi basari hizo zinatolewa na viongozi waliotwikwa jukumu hilo. Hivyo basi, Kaunti itatoa shilingi milioni 200 kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha pili hadi cha nne na wale wa kidato cha kwanza punde tu watakapojiunga,” alisema gavana huyo.
Wakati huo huo, aliyekuwa mbunge wa Kisauni Ali Mbogo ameikashifu serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kutowekeza vilivyo katika sekta ya elimu katika kaunti hiyo.
Akizungumza kwenye hafla ya ugavi wa basari kwa wanafunzi wasio na uwezo katika eneo la Barawa eneobunge la Kisauni, Bw Mbogo ambaye pia ni mwenyekiti wa mradi wa LAPSSET amesema ni jambo la kusikitisha kuwa serikali ya kaunti ya Mombasa kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu licha ya baadhi ya kaunti nyinginezo kutoka ukanda wa Pwani kuanza kupiga jeki sekta hiyo kikamilifu.
Mbogo vilevile amesema ni jambo la kusikitisha kuwa wanafunzi waliofanya vyema katika kaunti hiyo kuhangaika kutokana na kukosa ada za shule licha ya serikali kuweka hazina ya ustawi wa maeneobunge NGCDF.
Wakati huo huo, Bw Mbogo amewataka wakazi katika kaunti hiyo kuchagua viongozi waadilifu na watakaoangazia maslahi yao kikamilifu.