Kimataifa

UN yalaumiwa kwa kimya sana Gaza ikipondwa na Israeli

January 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

HALI ya wasiwasi imeibuka duniani kutokana na kimya cha Umoja wa Mataifa (UN), huku Israeli ikiendelea kutekeleza mashambulio makali dhidi ya Wapalestina katika ukanda wa Gaza.

Katika siku za hivi karibuni, Israeli imeongeza mashambulio yake katika ukanda huo, sasa ikizilenga hata taasisi za kibinadamu, kama vile hospitali kubwa, kama vile Al-Aqsa.

Ijapokuwa hapo awali, Israeli ilikuwa imeahidi kutozilenga taasisi za kibinadamu, hofu imeibuka kuhusu kimya cha UN, ikizingatiwa umoja huo umekuwa ukiingilia mizozo katika mataifa tofauti hapo awali, kama vile Kenya mnamo 2007/2008.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kisiasa na mahusiano ya kimataifa, kuna sababu kadhaa ambapo umoja huo umekuwa kimya, licha ya hali ya kibinadamu kuendelea kudorora Gaza.

Kulingana na Profesa Macharia Munene, ambaye ni msomi wa siasa za kimataifa, moja ya sababu ambazo zimechangia UN kunyamaza ni kuwa taifa hilo ni mshirika wa karibu wa Amerika.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’ Alhamisi, Prof Munene alisema Amerika na mataifa ya Magharibi kama Uingereza, Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa kati ya mengine ndiyo huwa yanatoa ufadhili mkubwa kwa umoja huo.

Hivyo, ikizingatiwa kuwa Israeli ni mshirika wa karibu wa Amerika, basi ni vigumu sana kwa marafiki wengine wa Amerika kujitokeza kumlaumu mshirika wake.

“Bila ufadhili kutoka kwa Amerika na mataifa mengine ya Magharibi, UN haijakamilika. Ni kama gari lisilo na petroli ya kutosha, au gari lisilo na injini. Kinaya kingine ni kuwa, mataifa mengi yenye usemi mkubwa katika umoja huo ni washirika wa Amerika. Hivyo, hayana budi ila kunyamaza na kutazama matukio yanayoendelea Gaza bila kuto sauti yoyote,” akasema Prof Munene.

Sababu nyingine ambapo umoja huo umenyamazia mashambulio hayo ni kuwa, kando na Amerika kutoa ufadhili mkubwa wa kifedha kwa UN, mataifa hayo pia hutegemea pakubwa misaada kutoka kwa Amerika.

Kulingana na Prof Munene, taasisi kubwa za kifedha, kwa mfano Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki Kuu ya Dunia, hudhibitiwa pakubwa na mataifa ya Magharibi.

Kinaya kingine ni kuwa, taasisi hizo ndizo zimekuwa zikitoa misaada mingi ya kifedha kwa mataifa yenye chumi za kadri, kama vile Kenya.

Machafuko baina ya Israeli na Hamas katika eneo la Gaza. PICHA | AFP

Hata hivyo, mdadisi huyo anaeleza kushangazwa na ushujaa wa kipekee ambao umedhihirishwa Afrika Kusini, kwani imeishtaki Israeli katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki (ICJ), kwa kuendeleza ukatili wa kibinadamu Gaza, Palestina.

“Afrika Kusini imeonyesha ushujaa wa kipekee kwa kuishtaki Israeli. Ni wazi kuwa taifa hilo lilifanya hivyo huku likifahamu ‘adhabu’ ambayo huenda likapata kutoka kwa Amerika na washirika wake. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba taifa hilo lina uungwaji mkono wa kichinichini wa mataifa kama Urusi na China-ambayo ni maadui wa Amerika na washirika wake,” akasema Prof Munene.

Wadadisi wanaeleza kwamba kutokana na migawanyiko mikubwa ya kisiasa iliyopo katika umoja huo, basi ni vigumu kwake kutoa sauti moja kukashifu ukatili unaoendelea Gaza.

“Hali ilivyo, makabiliano baina ya Israeli na wanamgambo wa Hamas yataendelea kushuhudiwa hadi pale Amerika itasuluhisha tofauti zake na mataifa kama China na Urusi. Kile tutaendelea kushuhudia ni sauti moja moja, kwa mfano kutoka mataifa ya Kiarabu, yakiwatetea Wapalestina. Sauti ya pamoja kutoka kwa UN ndiyo itasuluhisha hali ilivyo Gaza,” asema Prof Peter Kagwanja, ambaye pia ni msomi wa siasa za kimataifa.