Ndindi ndiye: Viongozi wamtaka Nyoro awanie urais 2032 badala ya Gachagua
NA MARTIN MWAURA
Ubabe wa kudhibiti siasa za Mlima Kenya umeongezeka kufuatia baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza kumtaka Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro awanie urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2032.
Viongozi hao wamemtaka Nyoro kuchukua uongozi wa taifa pindi baada ya Rais William Ruto kukamilisha hatamu yake wakisema ana tajriba ya kuongoza nchi.
Viongozi hao walisema Bw Nyoro ameafikia vigezo vyote vya kuwa rais huku Seneta wa Murang’a Joe Nyutu akisisitiza kwamba umewadia muda wa eneo hilo kumpata rais.
Semi hizo zinatazamiwa kuibua cheche za mdahalo na mgawanyiko zaidi katika eneo hilo la kati ambako Naibu Rais Rigathi Gachagua anachukuliwa kuwa mrithi wa Rais Ruto kutokana na nafasi kuu anayoshikilia serikalini.
Eneo la Mlimani liliachwa bila kigogo mwenye ushawishi mkubwa kufuatia kustaafu kwa Rais Uhuru Kenyatta baada ya uchaguzi wa 2022.
Bw Gachagua amekuwa akipanga mikakati ya kuibuka kuwa kigogo wa Mlimani, nafasi ambayo pia inamezewa mate na mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani) na Moses Kuria (Utumishi wa Umma) miongoni mwa wengine.
Viongozi hao wakiwemo Mbunge wa Mathioya Edwin Mugo, Wilson Sossion, Didmus Barasa (Kimilili) Muchangi Karemba (Runyenjes) Paul Biengo (Chesumei) Fred Ikana (Shinyalu), Jose Kiptoo (Emgwen) ambao walihudhuria hafla ya uzinduzi wa mradi wa Kiharu Masomo Bora, walisema Bw Nyoro anatosha kwa urais na kwamba anafaa kupewa nafasi.
Soma pia: Ndindi Nyoro: Sasa sio mchele na nyama tu, tumeongeza chapati na uji shuleni
Viongozi hao wa kisiasa walisema Bw Nyoro amekuwa akishiriki shughuli nyingi za kuunganisha viongozi.
Mbunge wa Gatundu Kusini Njoroge Kururia alisema hakukuwa na nafasi yoyote ya kuwaniwa katika eneo la Kati kwa sababu “alishamtawaza Bw Nyoro kuwa kigogo wa eneo hilo”.
“Hakuna kiongozi mwingine anayeweza kutupeleka mbele, ni Ndindi Nyoro pekee. Yeye ndiye ana vigezo vyote vya kuwa rais na wakati ule wakazi wa Kiharu watahitaji uungwaji wetu, tutakuwa hapa kumuunga mkono,” akasema.
Bw Mugo naye alimtaja Bw Nyoro kuwa kiongozi wa maono akimlinganisha na mpiganiaji wa demokrasia na mfumo wa vyama vingi Kenneth Matiba akisema kwamba alikuwa na uwezo wa kuipeleka nchi katika ufanisi mkubwa zaidi.
Alisema kwamba Bw Nyoro pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti na kwamba ameonyesha ujuzi mkubwa wa kusimamia rasilmali akirejelea miradi aliyotekeleza katika eneo hilo.
“Huyu ndiye Matiba wetu na tunaamini kwamba anaweza kuafikia yale ambayo [Matiba] hakuweza kufikia,” alisema Bw Mugo.
Naye Bw Nyutu alisema kwamba Bw Nyoro ni mwandani wa karibu wa Rais Ruto na kwamba alikuwa anajifunza mengi kutoka kwa kiongozi wa nchi na hivyo anatosha kurithi mikoba ya urais.
Na katika kile ambacho kinaweza kufasiriwa kama kijembe kwa Bw Gachagua, Bw Nyutu alisema mbunge huyo huwa rahisi kuanzisha urafiki na kwamba huwa tayari kufanya kazi na viongozi wengine, jambo alilosema ni muhimu mno kwa kiongozi wa kitaifa.
“Tuna imani na uongozi wako na uwezo wako wa kutupeleka mbele. Una kila kinachohitajika kuongoza taifa hili na hatuna shaka kwamba utatufikisha juu zaidi,” akasema Bw Nyutu.
Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Betty Maina naye alisema kwamba Bw Nyoro amefanya maendeleo makubwa kama mbunge na kwamba umewadia muda wake kufanya makubwa vile vile kitaifa.
“Tunakutaka uwe pale juu. Tunataka uwe Rais. Tunakuombea Mungu akupeleke juu hadi maadui wako washangae. Usisikilize kelele za wakosoaji wako na wale wasioamini uwezo wako kwa sababu wakati nyota yako inapoanza kung’aa utapata maadui wengi,” alisema akimtaka kukaa ngumu.
- Utafsiri: FATUMA BARIKI