Kimataifa

Hizi kashfa dhidi ya wahubiri maarufu kuendelea hadi lini?

January 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

KWA kawaida, maana na lengo kuu la dini huwa ni kutoa matumaini kwa washirika wake.

Dini huwa kama kimbilio la kumpa tumaini mwanadamu, kila mara anapokumbwa na changamoto za kimaisha.

Hata hivyo, mielekeo katika dini za kisasa imeanza kuibua maswali kuhusu ikiwa dini na viongozi wake bado wanaendelea kutekeleza jukumu muhimu la kuwa kimbilio kwa jamii.

Hili linatokana utata ambao umewakumba wahubiri wenye ushawishi mkubwa katika dini ya Kikristo katika siku za hivi karibuni, ambapo wengi wao wamekuwa wakihusishwa na vitendo vinavyokiuka ubinadamu na mafundisho ya vitabu vitakatifu.

Baadhi ya wahubiri ambao wamejipata kwenye utata huo ni marehemu TB Joshua kutoka Nigeria, Paul Mackenzie kutoka Kenya, ‘Pasta’ Victor Kanyari, marehemu Askofu Michael Njoroge, Askofu James Wahome katu ya wengine wengi.

Siku kadhaa zilizopita, ripoti moja ya kipekuzi ilifichua jinsi Mhubiri TB Joshua alikuwa akiwapumbaza wafuasi wake, ili kuamini kuhusu “miujiza” aliyokuwa akifanya.

Kwenye makala hayo, yaliyopeperushwa na kituo kimoja cha habari cha kimataifa, baadhi ya wafuasi wa kanisa la Synagogue Church of All Nations (SCOAN), walijitokeza na kueleza jinsi walikuwa wakipumbazwa na mhubiri huyo, ili kuamini kwamba walikuwa wameponywa magonjwa yao kutokana na ‘nguvu’ zake.

Kama hilo halitoshi, bintiye mhubiri huyo, anayeitwa Ajoke, alifichua jinsi aliteswa na babake (TB Joshua) kwa zaidi ya miaka  20.

“Watu waliomfuata walikuwa wamepewa maagizo makali kuhusu masharti ambayo wangefuata. Baadhi ya masharti hayo ni kumuita ‘Baba’, kutotumia simu wakiwa kanisani na kutoangalia maelezo yao ya kibinafsi, kama vile jumbe za barua pepe,” akasema binti huyo kwenye mahojiano na shirika hilo.

Ripoti hiyo ya kipekuzi inalingana na ufichuzi mwingine kumhusu Kasisi Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International Ministries, anayehusishwa na vifo tata ya watu waliopatikana wameuawa na kuzikwa katika eneo la Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Paul Mackenzie akiwa katika Mahakama ya Shanzu mnamo Juni 2, 2023. PICHA | WACHIRA MWANGI

Kulingana na video zinazoonyesha mahubiri ya Mackenzie siku za hapo nyuma, anaonekana akiwatahadharisha wafuasi wake dhidi ya kula au kunywa chochote.

“Mnafaa kutokula chochote ili kujitayarisha kwa ujio wa Kristo,” akasema.

Rioti zinaeleza kuwa kuna uwezekano kuwa baadhi ya wafuasi wake walifariki kuwa kuzingatia mafundisho ya kutokula chakula.

Marehemu Askofu Njoroge naye aligonga vichwa vvya habari mnamo 2010, baada ya kudaiwa kuwahonga baadhi ya washirika wake kukiri walikuwa wamepona baada yake kuwaombea.

Hata hivyo, mshirika mmoja alimwanika kwa wanahabari kwa “kutomlipa kama walivyokuwa wameagana”.

“Amekuwa akinilipa Sh2,000 kudanganya nimefungika mdomo, ila hayo ni uwongo. Nimeamua kujitokeza kumwanika baada yake kutonilipa kama tulivyokuwa tumekubaliana,” akasema mshirika huyo, aliyetambuliwa kama Esther Mwende.

Washirika wengine wamekuwa wakiwatetea vikali ‘wahubiri viongozi’ wao, kila mara wanapokosolewa kutokana na utata unaowakabili.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi na viongozi wa kidini wanasema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa makanisa yaliyopo nchini yamesajiliwa chini ya kanuni kali, ili kuepuka matukio kama hayo.

“Kenya inafaa kuiiga Rwanda, kwa kuhakikisha kuwa madhehebu yote—iwe ni katika dini za Kikristo, Kiislamu, Kihindi au kitamaduni—yamesajiliwa chini ya sheria kali. Hili litahakikisha matukio kama hayo hayashuhudiwi tena,” asema Kasisi (Profesa) Lawrence Njoroge, ambaye ni msomi wa masuala ya dini.