Habari Mseto

Kumbe basi lililoua abiria 15 lilikuwa na bima ya lori!

January 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WAMBUI

BASI lililohusika katika ajali mbaya ya barabarani Jumatano asubuhi katika eneo la Twin Bridge katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret lilikuwa na bima ya lori.

Hii inamaanisha familia zilizopoteza wapendwa wao huenda hazitafaulu kudai fidia kwa kufiwa na wapendwa wao.

Uchuguzi wa polisi katika eneo la tukio ulibaini kuwa dereva wa basi lililoendeshwa kwa kasi alikuwa akielekea Nairobi kutoka Kampala ambapo alipofika Twin Bridge, alishindwa kulidhibiti na kuingia upande wa kulia wa barabara na kuigonga moja kwa moja matatu ya kubeba abiria 14 nambari ya usajili KCJ 387S iliyoko chini ya North-ways Sacco .

Matatu hiyo ilikuwa ikielekea Eldoret kutoka Nakuru ajali hiyo ilipotokea na kuua watu wote waliokuwemo akiwemo dereva wake, watu wazima wanane na watoto saba walio na umri wa chini ya miaka 15.

Abiria 18 kati ya 45 waliokuwa katika basi hilo walipata majeraha madogo na walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Dereva wa basi hilo alitoroka eneo la tukio baada ya ajali hiyo lakini alikamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya Molo.

Kesi yake ikiendelea mahakamani, uchuguzi wa kibinafsi wa ajali hiyo umebaini kuwa basi hilo lililosajiliwa kwa nambari 6885AK05 lilikuwa likifanya kazi kinyume cha sheria chini ya bima isiyo sahihi, suala ambalo sasa limefikishwa katika Kitengo cha Uchunguzi wa Utapeli wa Bima cha Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA).

Basi hilo lilikatiwa bima na kampuni ya Invesco kama gari la biashara (lori) la abiria hadi watatu, ikimaanisha wakati wa ajali hiyo, lilikuwa likitumika kinyume cha sheria kama PSV, jambo ambalo lilikuwa nje ya kanuni ya bima.

Hii ina maana kuwa umiliki wa basi hilo ni wa ulaghai hasa ikizingatiwa kuwa kuna aliyeshirikiana na wafanyakazi katika kampuni ya Invesco Assurance Limited kupata bima isiyofaa.

Aliyekuwa mpelelezi serikalini na kwa sasa Mpelelezi wa Kibinafsi, Bw Daniel Muteshi alisema kuwa matokeo yake yamefichua kuwa stakabadhi zinaonyesha bima ilichukuliwa katika kampuni ya Invesco tawi la Tumaini jijini Nairobi mnamo Mei 2023 kwa takriban Sh9,000.