Habari Mseto

Mwanamume afungua ukurasa wa FB kwa jina la Mike Sonko bila idhini yake

January 14th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MWANAMUME aliyefungua ukurasa wa mtandao wa Facebook wa ‘kuchangisha pesa za kusaidia wahasiriwa mbalimbali’ akitumia jina la aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko bila idhini yake, ameshtakiwa.

Bw Newton Paul Kengere aliyefikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Gilbert Shikwe alishtakiwa kufungua ukurasa huo bila idhini ya Bw Sonko.

Bw Kengere alifungua ukurasa huo mnamo Septemba 15, 2023, akiwa kusikojulikana nchini Kenya.

Mshtakiwa huyo alifikishwa kortini mnamo Januari 12, 2024.

Alikana shtaka la kutumia jina la Bw Sonko kinyume cha sheria ya kudhibiti majukwaa ya mitandao ya intaneti nambari 28 ya uhalifu wa kimitandao iliyopitishwa mwaka wa 2018.

Katika ukurasa huo aliofungua Bw Kengere, aliupa jina la ‘Hon Mike Mbuvi Sonko Rescue Loans’.

Katika ule rasmi wa Bw Sonko, anautumia kutoa misaada kwa wale wanaokumbwa na maafa au matatizo mbalimbali kama vile ugonjwa, kifo na majanga mbalimbali.

Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko. PICHA | MAKTABA

Kwa muda mrefu, gavana huyo wa zamani wa Nairobi amekuwa akiwasaidia wahasiriwa wanaokumbwa na changamoto mbalimbali.

Mshtakiwa huyo aliomba hakimu amwachilie kwa dhamana akisema hatatoroka ila “nitafika kortini wakati wa kusikilizwa kwa kesi ama wakati ule mwingine wowote nitakapohitajika.”

Kiongozi wa mashtaka Bi Judy Koech hakupinga ombi la dhamana la mshtakiwa.

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu.

Bw Kengere alitiwa nguvuni Januari 11, 2024, na kufikishwa kortini Januari 12, 2024.

Mshtakiwa hakuweza kulipa dhamana hiyo mara moja na alipelekwa gereza la Industrial Area kuzuiliwa kule hadi pale atakapolipa dhamana ama kesi isikilizwe na kuamuliwa ndipo ama afungwe au aachiliwe.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili.