WANDERI: Uhuru na Raila, haki za waliofariki 2017 zi wapi?
Na WANDERI KAMAU
DAMU ya mwanadamu si ya mnyama. Ingawa mwanadamu hufananishwa na hayawani, maumbile yake huwa yenye upekee mkubwa.
Kulingana na mafunzo yaliyo katika misahafu, maumbile ya mwanadamu hufanana na ya Mwenyezi Mungu, ndipo akamuumba kulingana na mfano wake.
Funzo lingine ni kwamba, damu iliyomwagwa ‘hujililia’ na kulipiza kisasi yenyewe.
Natumia urejeleo huu kufuatia ziara ya Rais Uhuru Kenyatta katika Kaunti ya Kisumu, ambapo atapokewa na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kesho.
Kwenye ziara hiyo, Rais Kenyatta anatarajiwa kupokelewa vizuri kufuatia mwafaka wake wa kisiasa na Bw Odinga ambao ulimaliza taharuki ya kisiasa ambayo ilikuwa imeigubika nchi.
Wengi walifurahi kufuatia mwafaka huo. Waliusifu kwa kurejesha ‘utulivu’ wa kisiasa na utangamamo mpya miongoni mwa Wakenya.
Hata hivyo, viongozi hao wawili wamebaki kimya kuhusu mamia ya watu waliopoteza maisha yao kwenye makabiliano yao ya kisiasa katika chaguzi kuu za urais mnamo 2017.
Kitakuwa kinaya kwa Bw Odinga ‘kumkaribisha’ Rais Kenyatta katika eneo ambako Bw Odinga mwenyewe alishiriki katika hafla za kuchanga fedha kwa mazishi ya familia za watu waliofariki kutokana na ghasia za kisiasa.
Kitakuwa kinaya kikubwa kwa Rais Kenyatta ‘kufurahi’ katika eneo ambako polisi walitumia nguvu kuwatawanya na kuwaua waandamanaji ambao walishinikiza kuzingatiwa kwa haki yao ya kidemokrasia.
Ni kinaya kwa wawili hao ‘kucheka’ huku damu za Mtoto Pendo, Msichana Stephanie Moraa, Chris Msando, Jacob Juma kati ya wengine zikiitisha haki zikiwa bado makaburini. Ni kinaya kwa Rais Kenyatta kuwaambia Wakenya ‘kusahau yaliyopita na kuendelea na maisha yao’ huku mwanaharakati kama Miguna Miguna akiwa bado uhamishoni nchini Canada.
Katika jamii za Kiafrika, damu za watu waliouawa kikatili bila hatia zozote huwa zinalipiza kisasi kwa waliowaua. Ikiwa si hivyo, kisasi hicho hupitishwa katika kizazi kifuatacho, ikiwa watafariki bila wao kulipa gharama ya uhayawani waliotenda.
Ni kinaya katika nchi za Afrika au zile zenye ukuaji wa kadri kuwatakasa wanasiasa ama watu maarufu wanaotenda maovu na kuwaabudu kama ‘miungu wadogo.’
Ni kinaya kikubwa kwamba viongozi wanaohusika katika mauaji ya halaiki hutakaswa na kuonekana kama mashujaa wa jamii mbalimbali, huku waathiriwa wa dhuluma na ukatili wao wakionekana kama ‘wakosa’ waliohitaji kuadhibiwa.
Hii ni mojawapo ya sababu kuu ambazo zimekuwa zikitofautisha mifumo ya haki katika nchi zilizostawi kiviwanda na mataifa ya Afrika. Kwa mfano, nchini Ujerumani, washukiwa wakuu ambao walituhumiwa kushiriki katika mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi wakati wa utawala dhalimu wa Adolf Hitler bado wanasakwa.
Kesi za waliokamatwa zingali zinaendelea. Hii ni licha ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kuisha mnamo 1945; zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Funzo kuu ni kwamba lazima tuepuke kujitia hamnazo. Hatutaepuka mikosi ya kisiasa, ikiwa vilio vya wale waliofariki katika vita hivyo hawatatafutiwa haki. Tutazidi kuandamwa na mikasa. Wataendelea kudai haki.