Makala

AFCON 2019: Kenya ilivyopepeta Tanzania 3-2

January 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI 

MWAKILISHI wa kipekee wa Afrika Mashariki, Tanzania katika dimba la Klabu bora barani Afrika (Afcon) 2023 atashuka ugani dhidi ya Morocco Januari 17, 2024.

Timu hiyo ya taifa la Rais Samia Suluhu ikijulikana kama Taifa Stars chini ya ukufunzi wa Adel Amrouche kutoka Taifa la Algeria litaingia ugani saa mbili usiku.

Taifa hilo litarejea ugani Januari 21 dhidi ya Zambia saa tano usiku na tena Januari 24 dhidi ya DR Congo mwendo wa saa tano usiku.

Washindi wawili katika kundi hilo ndio wataungana na wengine 14 kuingia mechi za muondoano ili zibaki nane.

Hizo nane pia zitacheza awamu ya robo fainali, washindi waingie semi fainali ya kusaka wa kucheza fainali huku watakaoshindwa katika semi fainali wakicheza kusaka wa kutuzwa nambari tatu.

Tanzania imeshiriki michuano hiyo ambayo kwa sasa ni Makala ya 34 nchini Ivory Coast, mara mbili, 1980 na 2019.

Katika mara hizo mbili, taifa hilo lilitolewa katika awamu ya makundi, kwa ujumla ikipata pointi 1 kati ya zote 18 kwa kufunga mabao 5 huku nayo ikifungwa mara 14.

Ina maana kwamba taifa hilo linashiriki makala hayo kwa mara ya tatu sasa na pia limejihakikishia kushiriki 2027 kama mwenyeji wa dimba hilo pamoja na majirani Kenya na Uganda.

Mwaka wa 2019 Tanzania ilijipata katika kundi moja na Kenya, Algeria na Senegal ambapo tena iliibuka ya mwisho katika kundi hilo la C.

Tanzania ilipepetwa kwa magoli 3-2 na majirani wao Kenya, hali ambayo ilifanya imfute kocha wao Emmanuel Amunike.

Kando na Tanzania, mataifa mengine katika dimba hilo ni wenyeji Ivory Coast, Nigeria, Equatorial Guinea, na Guinea-Bissau katika kundi A huku kundi B likijumuisha Misiri, Ghana, Cape Verde na Mozambique.

Kundi la C lina Senegal, Cameroon, Guinea na Gambia huku kundi D likiwaleta pamoja Algeria, Burkina Faso, Mauritania na Angola huku kundi E likiwa na Tunisia, Mali, Afrika Kusini na Namibia.

[email protected]