Raila Junior: Nitakufa na Ruto 2027
ODINGA Junior ameapa kubaki katika chama cha ODM na kumuunga mkono Rais William Ruto katika azma yake ya kuchaguliwa tena mwaka ujao, licha ya tofauti za kisiasa zinazozidi kujitokeza katika familia ya Odinga.
Jana, Raila Odinga Junior aliungana na viongozi wakuu wa ODM na Waziri wa Madini Hassan Joho katika mkutano wa kumbukumbu ya Raila Odinga uliofanyika Garissa.
Haya yanatokea huku dadake Winnie Odinga akiendelea kuwakashifu baadhi ya maafisa wa chama hicho akidai walikodisha wahuni kuvuruga maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha baba yao yaliyofanyika katika uwanja wa Migwena, Bondo, wiki iliyopita.
“Aaah, inafurahisha sana kuwaona viongozi wote wazuri wa ODM wakiadhimisha kumbukumbu ya kwanza ya Baba.Walipokuwa Dubai, sisi tulipokea zawadi zao kutoka Afgoonistan! Asante. Ni lazima nasi tulipe kwa namna hiyo hiyo,” Winnie aliandika ujumbe uliofasiriwa kuwa kejeli katika ukurasa wake wa Instagram.
Aliambatanisha ujumbe huo na video iliyowaonyesha Waziri wa Madini Hassan Joho, Gavana wa Homa Bay ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi, Mbunge wa South Mugirango Silvanus Osoro, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed wakisafiri kwa ndege ya kibinafsi kutoka Eldoret hadi Garissa.
Mkutano wa Garissa ni miongoni mwa shughuli zilizoandaliwa na ODM katika kipindi cha “Mwezi wa Baba”, kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye aliongoza chama hicho kwa miaka 20.
Bw Junior, ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha ubunge cha Kibra, alisema atatumia tiketi ya ODM kuwania kiti hicho huku akipigia debe muhula wa pili wa Dkt Ruto.
Pia ameahidi kumuunga mkono ami yake Dkt Oburu Oginga, katika kukiongoza chama hicho.
“Nitabaki ODM hadi mwisho na nitaendeleza kampeni za kusaka uvumishaji Rais Ruto kote nchini anapotafuta kuchaguliwa tena, huku nikigombea ubunge wa Kibra kupitia ODM,” alisema katika mahojiano na Taifa Leo.
Alisema hataathiriwa na jamaa zake wanaochagua mwelekeo tofauti wa kisiasa, akisisitiza kuwa anajenga safari yake ya kisiasa mbali na kumuunga mkono Rais.
“Baba alituacha katika Serikali Jumuishi na hapo ndipo nitabaki. Nawarai watu wetu wamuunge mkono Rais achaguliwe tena. Nina Rais hadi mwisho,” akasema.
Kauli yake inajiri wakati ambapo tofauti zinaongezeka katika familia ya Odinga kuhusu mwelekeo wa ODM na ushirikiano wake na serikali ya Kenya Kwanza.
Shangazi yake, Mwakilishi wa Kike wa Kisumu, Ruth Odinga, amesema yuko tayari kuondoka ODM ikiwa kufanya hivyo kutasaidia kutetea haki na demokrasia.
Akizungumza katika uwanja wa Migwena wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha kaka yake, alisema, “Ikiwa kusimama na ODM kunamaanisha kujitolea kila kitu kulinda haki, basi iwe hivyo. Nikilazimika kujiunga na chama kingine ili kuhakikisha haki inapatikana Kenya, nitafanya hivyo.”
Winnie naye amekosoa baadhi ya misimamo ya uongozi wa ODM na kutangaza kuwania kiti cha useneta wa Nairobi kinachoshikiliwa na Edwin Sifuna.
“Isiwe uvumi tena; Edwin Sifuna anapotafuta wadhifa wa juu, mimi nimeona nafasi. Ndiyo maana nitawania useneta wa Nairobi. Hata hivyo, sitaenda peke yangu; ninaenda na vijana,” akasema.
Kuhusu azma ya Winnie, Bw Junior alisema ana haki ya kidemokrasia kuwania kiti hicho lakini akamtaka kutafuta tiketi ya ODM kwa kushindana na Mbunge wa Lang’ata, Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o, katika uteuzi wa chama.
Bw Junior amekuwa akimuunga mkono Jalang’o, akisema ODM inapaswa kumuunga mkono atakayeshinda uteuzi.
Tofauti hizo pia zimeibua mjadala kuhusu nani anayefaa kuendeleza urithi wa kisiasa wa Raila.
Bw Junior alipinga hatua ya baadhi ya wazee wa jamii ya Luo kumtawaza Winnie kuwa mrithi wa kisiasa wa babake. Siku ya kutawazwa kwa Bi Winnie, Bw Junior na Jaoko Oburu, anayelenga ubunge wa Bondo, walikutana na Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya, aliyeahidi kuwaunga mkono kisiasa.
Bw Junior pia amemtetea mamake Ida Odinga dhidi ya ukosoaji kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, akisema kamati ilihusika na mialiko kwa kushauriana na familia.