Habari Mseto

Maina Njenga: Mimi si wa kuwatuma vijana wanyang’anyi waniletee pesa

January 17th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi la Mungiki, Bw Maina Njenga, amekanusha madai kwamba kundi hilo limefufuka upya na limekuwa likiendesha uhalifu katika maeneo tofauti ukanda wa Mlima Kenya.

Mnamo Jumatano, Bw Njenga alitaja madai hayo, ambayo yamekuwa yakienezwa na baadhi ya viongozi, kama vile Naibu Rais Rigathi Gachagua, kama “propaganda na njama za kuwapaka tope vijana katika eneo hilo”.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatano, Bw Njenga alisema amekuwa akifanya kazi kwa miaka 36—tangu 1987—hivyo hawezi kuwatumia vijana kutekeleza uhalifu au kuwanyang’anya watu mali yao na baadaye kumletea.

“Mimi nina mali yangu. Nimekuwa nikifanya kazi kwa zaidi ya miaka 30. Siwezi kuwatuma vijana kuwanyang’anya watu mali yao na baadaye kuniletea,” akasema mwanasiasa huyo, kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Inooro FM.

Kauli hiyo imekuwa ikitolewa na Bw Gachagua, kwamba kundi hilo limefufuka upya, na limekuwa likiendesha uhalifu katika ukanda huo.

Lakini Jumatano, Bw Njenga aliata madai hayo kuwa uvumi mtupu, unaotejelea matukio yaliyofanyika zaidi ya miaka 20 iliyopita.

“Kundi hilo halijafufuka. Wanaosema hivyo wanarejelea matukio yaliyofanyika miaka mingi sana. Vijana wanaojitokeza katika maeneo tofauti wanafanya hivyo kwa kukosa ajira. Hivyo, badala ya viongozi hao kuwapaka tope vijana wetu, wanafaa kuwatafutia ajira,” akasema Bw Njenga.