Polisi watibua maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi DRC
Na MASHIRIKA
KINSHASA, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
POLISI nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumanne waliwatawanya waandamanaji jijini humu wakipinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliofanyika Desemba 2023.
Wafuasi wapatao 50 chama cha Movement for the Liberation of Congo (MLC) walioandamana kupinga idadi ya viti ambavyo chama hicho kilishinda katika uchaguzi huo.
Waliteketeza magurudumu na kutamka maneno ya kuikashifu Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) kabla ya polisi kufika na kucharaza washiriki kisha kuwakamata wengine.
Waandamanaji walisema idadi ya wabunge wa MLC katika Bunge la Kitaifa haiakisi jinsi chama hicho kilifanya katika uchaguzi huo.
Chama cha MLC, kinaongozwa na Waziri wa Ulinzi Jean-Pierre Bemba—mshirika wa Rais Felix Tshisekedi- na ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano tawala.
Chama cha UDPS chake Tshisekedi kilishinda viti 69 katika uchaguzi huo wa ubunge, viti 35 zaidi ya vile ambavyo kilipata katika uchaguzi wa 2018.
Chama cha MLC kilishinda viti 19, vikilinganishwa na viti 17 katika uchaguzi wa 2018, kulingana na matokeo ya muda yaliyotangazwa wiki hii.
Vyama vya upinzani nchini DRC vimeendelea kukashifu uchaguzi huo kwa kuutaja kama uliosheheni udanganyifu. Vimetaka uchaguzi huo urudiwe, ombi ambalo limepingwa na serikali.
Hali ya kutoelewana iliyotokea kutokana na uchaguzi huo unatishia kusababisha misukosuko zaidi katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini.
Aidha, migawanyiko ndani ya muungano tawala wa Sacred Union Coalition (SUC) uliokuwa na viti 390 katika bunge lililopita huenda ikahatarisha mpango wa Rais Tshisekedi wa kuunda serikali mpya thabiti na yenye idadi kubwa ya wabunge katika bunge la kitaifa.
Kiongozi mmoja wa chama cha MLC, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema anahisi kuwa chama hicho kimeshinda idadi ndogo zaidi ya viti kinyume na matarajio yake.