Kimataifa

Mkenya azuiliwa Marekani kwa kudaiwa kumuua muuzaji kuni

January 21st, 2024 2 min read

NA RUTH MBULA

RAIA wa Kenya anayeishi Fort Worth, Texas Marekani, alikamatwa na kuzuiliwa kwa tuhuma za kumuua mwanamume ambaye alimuona akipeleka kuni kwa jirani yake.

Christantus Omondi, 27, anadaiwa kupandwa na mori na kutoka nyumbani kwake akiwa uchi kisha kumuua mwanamume huyo ambaye alikuwa amemletea jirani yake kuni.

Bw Omondi ameshtakiwa kwa mauaji na pia kumjeruhi mlinzi na kumzuilia kutekeleza wajibu wake. Anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha urekebishaji tabia baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50 milioni.

Tukio hilo lilifanyika kipindi hiki msimu wa baridi unapoendelea kushuhudiwa mashariki mwa Amerika huku watu zaidi ya 30 wakiaga dunia kwa kulemewa na baridi.

Jirani ya Bw Omondi ambaye hakutaka jina lake linukuliwe na vyombo vya habari, alikuwa amemkodisha marehemu amletee kuni ili kujizuia kukabiliwa na baridi kali ndani ya nyumba yake.

Hata hivyo, mambo yaligeuka baada yao kuvamiwa na Mkenya huyo akiwa uchi na katika njia isiyoeleweka.

“Dereva aliyekuwa amepeleka kuni alipigwa hadi kufa na mwanamume ambaye alikuwa uchi,” stakabadhi za korti zilieleza.

Polisi jijini Texas walithibitisha kisa hicho na kusema baada ya tukio hilo, alienda kwa nyumba nyingine ambayo alikuwa amekodisha na kutishia kumuua mtu mwingine ambaye alikuwa akiishi karibu na chumba hicho.

“Marehemu alikuwa akitekeleza wajibu wake wa kuwasilisha kuni kwa mteja wake kwenye makazi ya Fort Worth. Mmiliki wa nyumba alijitokeza kuja kumsaidia,” wakasema polisi.

Mmiliki wa nyumba alifanikiwa kuhepa na anasema Bw Omondi alikuwa anaonyesha ukali na hasira ya kumuumiza mtu yeyote.

Aliyekuwa amepelekewa kuni aliwaambia wanahabari jijini Dallas kuwa Bw Omondi alikuwa akilenga kuwaua wote.

“Naamini rohoni mwangu kuwa alikuwa ametumwa atuue,” akasema.

Baada ya polisi kuitwa nyumbani mwake, walimpata Bw Omondi akiwa bado uchi na inashangaza kuwa kijibaridi nacho kilikuwa kikali. Walipompata, walimnyaka kwa kumtia pingu na kuenda naye.

Maafisa hao walimpata dereva huyo Scotty Jackson,51, akiwa amefariki akiwa amepigwa kwa kifaa butu kwenye shingo hadi kichwani.

Rekodi zinaonyesha kuwa si mara ya kwanza ambapo Bw Omondi anajihusisha na masuala ya uhalifu. Amewahi kuhepa kukamatwa na pia anashutumiwa kwa kumwelekezea afisa wa usalama bunduki.