Magavana walia kucheleweshewa fedha
NA COLLINS OMULO
HUENDA shughuli zikalemazwa katika kaunti mbalimbali baada ya serikali ya kitaifa kukosa kutuma zaidi ya Sh80 bilioni ambazo kaunti zote 47 zinastahili kupokea.
Baadhi ya kaunti tayari zimeshindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara na pia zimekosa kuwasilisha makato yao kwa asasi mbalimbali kwa muda wa miezi mitatu iliyopita.
Haya yanajiri wakati ambapo Baraza la Magavana Nchini (CoG) nalo limekataa pendekezo la kaunti zigawiwe Sh391. 14 bilioni mwaka huu wa kifedha.
Kaunti zinataka kiasi hicho kiongezwe hadi Sh450 bilioni.
Kwa mujibu wa CoG, magavana wanadai serikali kuu mgao kutoka Novemba 2023.
Kaunti hazijapokea mgao wa Desemba na Januari.
Mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru amesema kaunti 24 zinadai serikali kuu Sh17.48 bilioni kama mgao wa Novemba ambapo kaunti zote zilistahili kupokea jumla ya Sh32.761 bilioni.
Kaunti ambazo hazijapata mgao wao wa Novemba ni Siaya, Bomet, Busia, Bungoma, Embu, Garissa, Kiambu, Kilifi, Kisii, West Pokot, Wajir, Vihiga, Turkana, Trans Nzoia, Tana River, Nyeri, Taita Taveta, Kwale, Samburu, Machakos, Makueni, Lamu na Kitui.
Pia, kaunti 47 zinadai serikali kuu Sh30.83 bilioni ambazo ni mgao wa Disemba 2023 na Sh32.76 ambazo ni mgao wa Januari 2024.
“Tunasikitikia kucheleweshwa kwa mgao wa pesa za kaunti kwa miezi mitatu iliyopita. Kufikia Januari 19, 2024, Hazina Kuu bado haikuwa imesambaza Sh81.08 kwa kaunti kulingana na sheria ambazo zilipitishwa na Bunge la Seneti,” akasema Bi Waiguru.
Kulingana na Sheria za Kudhibiti Matumizi ya Pesa za Umma, Hazina Kuu ya Kifedha inastahili kutumia kaunti mgao wake wa kila mwezi, kati ya tarehe 1 hadi tarahe 15.
Alipochukua hatamu ya uongozi baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, Rais William Ruto aliahidi kuwa kaunti sasa hazitakuwa zikicheleweshewa mgao wao.
Magavana nao wamekuwa wakisema kucheleweshwa kwa pesa hizo kumetatiza juhudi zao za kupambana na majanga mbalimbali kama mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa nchini kutokana na mvua ya El Nino.
“Tunaomba Hazina Kuu itoe Sh81.08 bilioni ambazo zinastahili kuelekezwa kwa serikali za kaunti,” akasema Bi Waiguru ambaye pia ni Gavana wa Kirinyaga.
Kaunti zinastahili kupokea Sh32.761 bilioni mnamo Februari 2024, Sh30.833 bilioni kisha Sh34.68 bilioni na Sh30.83 bilioni mtawalia.
Tume inayosimamia mgao wa pesa zilizokusanywa (CRA) na Hazina Kuu zimekubaliana kuwa Sh398.14 pekee ndizo zitumwe kwa kaunti hadi mwaka wa fedha unaotamatika mnamo 2025.
Kwa upande mwingine, CoG nayo inasisitiza kuwa hawatakubali chochote chini ya Sh450 bilioni.
“Hili ndilo pendekezo pekee ambalo linakubalika kikatiba. Tunatoa wito kwa Hazina Kuu ya Kifedha na Bunge la Kitaifa kuliidhinisha ili kaunti zijimudu kifedha kutekeleza wajibu wake,” akaongeza Bi Waiguru