• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Magavana waitia presha serikali kuu itoe pesa za mgao wa bajeti kwa wakati

Magavana waitia presha serikali kuu itoe pesa za mgao wa bajeti kwa wakati

NA CHARLES WASONGA

MAGAVANA wamefufua mvutano kati yao na serikali ya kitaifa kuhusu kucheleweshwa kwa fedha za mgao wa bajeti kwa kaunti hizo.

Wanadai Hazina ya Kitaifa bado inashikilia kima cha Sh81 bilioni ambazo ni mgao wa miezi ya Novemba na Desemba 2023 na Januari 2024.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Ijumaa, mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (CoG) Anne Waiguru alisema pesa hizo zinawakilisha mgao wa Sh17.48 bilioni za Novemba 2023 ambazo kaunti 24 zinadai, Sh30.83 bilioni za Desemba 2023 ambazo kaunti 47 zinadai na Sh32.76 bilioni za Januari 2024 ambazo kaunti 47 zinadai.

“Kucheleweshwa kwa pesa hizi kumeathiri uwezo wa serikali za kaunti kushughulikia masuala ya dharura kama malipo au fidia kwa waathiriwa wa mafuriko katika sehemu mbalimbali nchini,” Bi Waiguru akasema.

“Aidha, kucheleweshwa kwa pesa hizo kutachangia serikali zetu kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi na kuwasilisha kwa pesa zinazokatwa wafanyakazi kuelekezwa kwa hazina mbalimbali. Kwa hivyo, tunaitaka Hazina ya Kitaifa kutoa Sh81.08 bilioni ambazo serikali za kaunti zinadai bila kucheleweshwa,” akaongeza Gavana huyo wa Kirinyaga.

Bi Waiguru alisema hayo baada ya kuongoza mkutano wa kwanza wa magavana wote mwaka huu wa 2024.

Rais William Ruto amekuwa akijidai kuhusu namna serikali yake ndiyo imekuwa ikitoa pesa zote kwa serikali za kaunti kwa wakati.

“Hii inaonyesha kuwa Kenya Kwanza imejitolewa kufaulisha ugatuzi,” Dkt Ruto akasema mnamo Desemba 12, 2023, wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 60 tangu Kenya kupata uhuru.

Wakati huo huo, magavana hao 47 wamependekeza kuwa serikali za kaunti zitengewe Sh450 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

“Hili ndilo pendekezo ambalo linawezekana mwa mujibu wa Katiba. Kwa hivyo, tunaitaka Hazina ya Kitaifa na Bunge la Kitaifa kuidhinisha pendekezo la CoG ili kuziwezesha serikali za kaunti kuendesha majukumu yao bila tatizo lolote,” Bi Waiguru akasema.

Bi Waiguru amekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana tangu Septemba 17, 2022.

Soma Pia: Waiguru achaguliwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke aliyepata mimba akiwa kwenye ibada za Shakahola...

Refarii wa Kombe la Dunia afunga mkewe bao la mapenzi

T L