AKILIMALI: Teknolojia yamwezesha kuangua watoto wa samaki bila masihara
NA FAUSTINE NGILA
AKILIMALI inapofika kwake, inampata George Muga akiweka paneli la kunasa kawi ya jua nje ya nyumba yake.?Kisha, kwa umakini, analiunganisha kwa jenereta ambayo nayo imeunganishwa kwa waya kwa pampu ya maji.
Baadaye, anaiwasha jenereta ile na pampu kisha maji kutoka mto ulio karibu yanaanza kutiririka hadi kwa kidimbwi chake anamofugia samaki.
Muga, ambaye anaenzi ufugaji wa samaki, amewekeza kwa uanguaji wa chengu (watoto wa samaki) eneo la Kendu Bay, Kaunti ya Homa Bay, anaweza kuhakikisha maji katika kidimbwi chake ni safi bila kugharamika kwa bili za umeme.
Kutoka mtoni, maji hayo hupitia kwa kichujio kilichoundwa kutokana na kibuyu kilichojazwa changarawe na vijiwe hadi kati.?Vijiwe hivi husaidia kusafisha yale maji na kuondoa uchafu kabla ya kuingia kwa mfumo wake wa kiteknolojia anaotumia kuangua chengu.?Mfumo huu kwenye viwanda na maduka unaweza kumgharimu mfugaji mamilioni ya hela, huku bei yake ikiongezeka baada ya sheria mpya ya ushuru.
“Mayai ya samaki katika kiangulio yanahitaji maji safi kutiririka bila kukatika. Kuhakikisha ubora wa juu wa maji, mfumo huu wa kujitengenezea huondoa uchafu kwa mbinu ya kichujio,” anasema.
Kutokana na uvumbuzi huu, mfugaji huyu mwenye umri wa miaka 48 anaweza kuangua zaidi ya chengu 100,000 wa Tilapia kila mwezi. Anauza kila chengu kwa Sh5 na Sh7 kulingana na ukubwa.
Yeye ni mhasibu, lakini aliamua kujitosa kwa ufugaji wa samaki miongo miwili iliyopita kwa mtaji wa Sh22,000, hela ambazo alikuwa amehifadhi kutokana na mshahara wake wa uhasibu.
Hapo 2002, miaka michache kabla ya kuwekeza kikamilifu kwa biashara hii, alimiliki vidimbwi viwili vya mita 10 mraba nyumbani kwake katika kijiji cha Awach.
“Nilianza kwa chengu 500 aina ya Catfish nilionunua kwa Sh4 kila mmoja kisha nikachimba na kuunda kidimbwi cha kufugia,” anaeleza.?Hata hivyo, baada ya taarifa kuenea kuwa alikuwa na samaki waliokomaa, alianza kupokea oda za chengu.?Kutokana na uvuvi wake, aliuza samaki 200 kwa Sh200 na kutia mfukoni Sh40,000 kutokana na uvuvi wake wa kwanza. Changamoto sasa ikaingilia juhudi zake.
“Nilikuwa ninanunua chengu kutoka kwa viangulio mjini Kisumu lakini kwa sababu ya ukosefu kutokana na ufugaji kwa wingi, ilikuwa inanibidi nisubiri kwa siku kadhaa kabla ya kupokea oda zangu. Nilichoshwa na subira hiyo, na nikaamua kuanzisha kiangulio changu mwenyewe,” anasimulia.
Kujenga kiangulio hicho cha mita tano kwa nne, Muga alitumia Sh65,000. Mayai yake huchukua muda wa siku tatu hadi nne kuanguliwa.
Mfugaji huyu amehudhuria vikao vingi vya mafunzo kunoa maarifa yake katika biashara ya uanguaji wa chengu, kikiwemo kimoja cha Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
“Wakati FAO ilizuru shamba langu la vidimbwi hapo 2014, waliniuliza iwapo nilikuwa nimewazia kuangua chengu ili kuimarisha mapato yangu. Nilipata motisha na kuingia biashara hiyo bila wasiwasi,” anaelezea.
Kwa sasa, anamiliki vidimbwi vinne vya mita 300 mraba kando na kiangulio. Katika kila kidimbwi, anafuga Tilapia wapatao 1,000 ambao huchukua miezi minane kukomaa.?Anauza kilo moja ya Tilapia kwa Sh350 huku samaki wengi akiwauza kwa kati ya Sh120 na Sh150 kila mmoja.?Muga, ambaye sasa ndiye mwenyekiti wa shirika la Ufugaji wa Samaki la Homa Bay anafichua kuwa yeye huwafundisha wanachama wa shirika hilo kuhusu uzalishaji wa samaki na teknolojia bora husika, anasema kuwa changamoto kuu katika biashara hiyo ni Tilapia kuliwa na wanyama wa nje.
Katika vidimbwi vya chengu, Muga anashauri kuwa ni muhimu kuhakikisha kuna maji safi ya kutosha yenye algae.?“Wafugaji wa samaki wanafaa kuhakikisha wamefuatilia usafi wa maji kwa kuthibitisha kuwa maji hayana rangi nyeusi na wakati ambao samaki wanahitaji kuelea majini.”
Arnoud Meijberg, afisa katika Mpango wa Ufugaji wa Samaki kwa ajili ya Sokoni nchini (KMAP) anaeleza kuwa kuongeza uzani wa kukuza chengu hadi gramu tano na zaidi hupunguza kiwango cha vifo, muda wa uzalishaji na gharama za uwekezaji.
Anawashauri wafugaji kutolemewa kujitosa kwa biashara ya uanguaji wa chengu kwa sababu ya ughali wake, kwa kuwa wanaweza kutumia teknolojia za kinyumbani kama Bw Muga.