Afya na Jamii

Wanaume wenye matiti makubwa wamo katika hatari ya kufariki mapema

January 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

WANAUME ambao wana matiti ambayo yametanuka (gynecomastia), wapo katika hatari ya kufa kabla ya kufika umri wa miaka 75, Wanasayansi wamebaini.

Watafiti walifichua kuwa wanaume ambao wana maradhi kama saratani, matatizo kwenye mapafu ambayo hayajagunduliwa na magonjwa mengine sugu wapo katika hatari zaidi kufa iwapo wana matiti ambayo yametanuka.

Mwanaume kuwa na matiti makubwa huwa kunasababishwa na kutosawazishwa kwa homoni muhimu ndani ya mwili. Hali hii inawaathiri theluthi mbili ya wanaume wote duniani japo ni kulingana na umri.

Watafiti kutoka Denmark kwenye jarida la BMJ Open walibaini kuwa tatizo la matiti kuwa makubwa kwa wanaume hukolea sana hasa wakiingia uzeeni.

Huku homoni za kiume nazo zikipungua uzeeni, wanaume wengi huanza kuongeza huzani ambao huhatarisha hali kwa matiti kuongezeka ukubwa.

Katika utafiti huo, ilibainika kuwa wanaume ambao wana matatizo ya afya mapema wakati wa uhai wao kabla ya kutinga uzeeni, wapo kwenye hatari ya kupatwa na tatizo la matiti kutanuka.

Wakati wa utafiti huo, ilibainika kuwa wale ambao wana matiti makubwa wako kwenye hatari ya kufa kabla ya kutinga miaka 75 kwa sababu kinga ya mwili wao hudhoofishwa na magonjwa yanayowasibu.

Kuepuka hali hiyo, wanapendekeza kuwa wale ambao wana matatizo mbalimbali ya afya wawe wakifuatilia hali yao na kupokea matibabu mapema.

Hii ni kwa sababu kutanuka kwa matiti huhusishwa sana na matatizo ya baadaye ya afya hasa uzee ukibisha.

“Wanaume ambao wana matiti yaliyotanuka wapo katika hatari ya kufa kwa asilimia 37. Hoja hapa ni kuwa lazima wawe wanatatizwa na magonjwa mengine yanayolemaza kingamwili yao. Hii ndiyo maana kila mmoja anastahili kupitia uchunguzi wa ndani wa afya kila mara kufahamu magonjwa yanayomwandama na kupokea matibabu,” wakasema watafiti hao.