Rais mkongwe wa Liberia nusura azirai akisoma hotuba ya kiapo
NA LABAAN SHABAAN
RAIS wa Liberia Joseph Boakai alishindwa kuhimili jua kali la Monrovia nusura azirai alipokuwa anasoma hotuba baada ya kuapishwa kuongoza nchi hiyo mnamo Jumatatu Januari 22, 2024.
Unyonge wa Rais Boakai mwenye umri wa miaka 79 ulidhihirika dakika 30 ndani ya harakati ya kuhutubu aliposita ghafla.
Ilibidi wasaidizi wake wakurupuke na kumpepetea hewa safi.
Ijapokuwa hatimaye alimaliza kusoma hotuba, Rais Boakai alihangaika sana kumalizia.
Hapo ndipo hafla ya kiapo kilikatizwa kabla ya wakati ulioratibiwa na Rais kuondoka jukwaani.
Hili si tukio la ajabu kwa Liberia sababu Rais huyu amekuwa akikejeliwa na mahasimu wake wa kisiasa na kuitwa “Sleepy Joe” kurejelea hulka yake ya kuonekana amelala hadharani.
Ndiye Rais mzee kabisa katika historia ya orodha ya viongozi wa nchi Liberia.
Bw Boakai alishinda kura za urais Novemba 2023 licha ya kutaniwa na wapinzani na watumiaji mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akisinzia katika mikutano ya hadhara.
Lakini wandani wake hupinga madai haya wakisema macho yake huwa madogo na kope huning’inia hivyo huonekana kama amelala.
Ili kupamba muonekano wake, Bw Boakai aliamua kuvalia miwani mieusi katika misafara ya kampeini.
Hata hivyo, hali yake ya afya imetiliwa mashaka hasa ikizingatiwa atamaliza awamu yake ya uongozi akiwa na umri wa miaka 85.
Kujibu pingamizi dhidi ya hali yake, Bw Boakai alisema Liberia imepata baraka kuwa naye akiwa na umri mkubwa sababu hali hii huja na maarifa na uwajibikaji.
“Achia mbali mambo ya afya, umri wangu ni baraka kwa nchi,” alisema Rais mwenye matatizo ya moyo alipohojiwa na kituo cha habari cha Uingereza BBC.
Rais Boakai anachukua hatamu za uongozi kutoka kwa Rais mchanga zaidi George Weah, 51, baada ya kumpiku kwa kura zaidi ya 20,000 katika uchaguzi wa duru ya pili.