AKILIMALI: Spinachi ya majani makubwa inayovunwa miaka 2 mfululizo
Na SAMMY WAWERU
Maonyesho ya kilimo yaliyofanyika Mariira Farm, kaunti ndogo ya Kigumo, Murang’a Septemba 2018 yalihudhuriwa na wataalamu na wakulima kutoka dira tofauti za taifa.
Ilikuwa fahari kwa wanazaraa kupata mwanya wa kuonyesha na kunadi mazao na jitihada zao katika kilimo, huku wataalamu wakitoa mafunzo maalumu pamoja na ushauri kuhusu sekta nzima ya kilimo.
Ni maonyesho yaliyotumika kunoa makali wakulima limbukeni, waliobobea wakiongezewa maarifa.?Ni kupitia maonyesho hayo ambapo kampuni ya Safari Seeds ilitumia fursa hiyo kuwasilisha Spinachi ya aina yake, yenye majani na matawi makubwa.
Kinyume na spinachi zingine, Giant Ford Hook, ambayo ni geni katika soko la kilimo, hustawi katika mchanga au udongo wowote ule.?Caroline Njeri ni mtaalamu wa masuala ya kilimo wa Safari Seeds na anasema haibagui inakokuziwa.
“Inachohitaji ni maji pekee. Spinachi zingine hubagua aina ya mchanga,” anadokeza.?Kulingana naye ni kwamba spinachi hii inastawi katika eneo lolote la nchi hii, almuradi inapata maji ya kutosha. Aidha, inaweza kupandwa katika eneo tambarare (open field) ama kwenye vifungulio (green house).
Hata hivyo, ili kupunguza gharama Njeri anapendekeza ikuzwe katika eneo tambarare. Sawa na spinachi kama King of Denmark, New Zealand, Bloomsdale Long Standing, Giant Noble, Early Hybrid No. 7 na Swiss Chard, Giant Ford Hook imesheheni vitamini C na haina asidi yoyote. Hali kadhalika, matawi na majani yake ni mwororo na tamu.
Kwa mujibu wa Njeri ni kuwa upanzi na utunzaji wake ni rahisi mno, kwa kuwa miche yake inachukua muda wa kati ya wiki 3-4 pekee. Mshauri huyu wa kilimo anasema kwa sababu majani yake ni makubwa, nafasi ya shimo hadi lingine iwe sentimita 30.
“Laini ya mashimo hadi nyingine iwe na upana wa kati ya sentimita 30-45,” afafanua.?Upandaji wa mboga hii unahitaji mbolea hai kama vile ya mifugo au kuku, lakini Njeri anasema inaweza ikachanganywa na ya kisasa. Wakati wa mahojiano, aliambia Akilimali kuwa ekari moja inasitiri gramu 500 za mbegu za Giant Ford Hook.
“Huchukua muda wa siku 30 pekee kuwa tayari kwa mavuno,” alisema.?Ili kupata mavuno tele, aina hii ya spinachi hutunzwa kwa maji maeneo yanayoshuhudia ukame, ilhali yenye mvua mkulima akikadiria faida tupu.
Vilevile, palilizi ni jambo la muhimu kuzingatia ili kukabiliana na kwekwe.?Kuna aina tofauti ya mbolea za kisasa za kustawisha mazao, ambazo mkulima anapendekezwa kuwa akizitia mara moja kwa mwezi kwenye mashina ya Giant Ford Hook.
“Mbolea kama Urea, CAN au NPK husaidia kuongeza mazao na pindi iwekwapo mimea inyunyiziwe maji ya kutosha,” ashauri mtaalumu huyu.?Sawa na mboga zingine, spinachi hii pia hushambuliwa na wadudu kama; Viwavi, vidukari na konokono. Mnyauko, ukungu na virusi vinavyosambazwa na wadudu ni baadhi tu ya magonjwa yanayoathiri Giant Ford Hook.?Hata hivyo, Njeri anashauri haja ya mkulima kupata maelekezo kamilifu kutoka kwa mtaalamu wa kilimo dhidi ya wadudu na magonjwa.
“Mmea ukionyesha dalili za virusi unapaswa kung’olewa mara moja ili usiambukize mingine,” ashauri.?Anaeleza kuwa ekari moja huzalisha kati ya tani 20-30 za spinachi hii kwa wiki. Giant Ford Hook huvunwa kwa muda wa miaka miwili mfululizo, kabla ya kukamilisha uzalishaji wake.
Soko la mboga hutegemea msimu na maeneo zinakokuzwa. Ili kuepuka kero la kupunjwa na mawakala, wataalamu wa masuala ya kilimo na biashara wanashauri mkulima kufanya utafiti wa kutosha kujua soko la mazao yake kabla ya shughuli za mavuno kuanza.
Pia, kujisajili katika vyama vya ushirika (Sacco), kuzalisha bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo, kufanya matangazo kupitia mitandao na vyombo vya habari ni baadhi ya njia zinazomuwezesha mkulima kupata wateja wa moja kwa moja.