Habari Mseto

Wanaume watano wapatikana na hatia ya kuiba Sh15m kimabavu

January 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

WANAUME watano waliomnyang’anya mkurugenzi wa kampuni ya kuuza kompyuta takriban Dola 150,000 (sawa na Sh15 milioni mwaka 2020) wakitishia kumuua kwa kumpiga risasi, wamepatikana na hatia ya kutekeleza wizi kimabavu.

Hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Bernard Ochoi aliwapata Walter Keverenge, Bernard Ogutu Oketch, Albert Okech Ochola, Wycliffe Mbarani Mukuviza, na George Onyango Mitere wakiwa na hatia ya kumnyang’anya kimabavu Daksha Patel pesa hizo.

“Mkiwa mmejihami na bastola mlimnyang’anya Bw Patel takriban Dola 150,000 ambazo ni sawa na Sh15 milioni mnamo Desemba 7, 2020,” Bw Ochoi alisema akipitisha hukumu.

Thamani ya pesa hizo mwaka 2024 ni Sh24 milioni kutokana na kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya Dola ya Marekani.

Alisema washtakiwa hao walimkabili Bw Patel ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya kuuza Kompyuta ya Mitsumi Business Park Computer Garage Limited (MBPCGL) mwendo wa saa kumi na moja jioni na kumtishia maisha kwa bastola.

Pia walimtandika mateke na kumnyeshea masumbwi mazito kabla ya kutoweka na kitita hicho za pesa za kigeni.

Hakimu alisema baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulioongozwa na James Gachoka, amefikia uamuzi kwamba washtakiwa walitekeleza uhalifu huo.

Washtakiwa walijitetea na kuomba waonewe huruma kwa vile wako na familia changa zinazowategemea.

Keverenge alifichua kwamba alikuwa msimamizi wa wafanyakazi katika kampuni hiyo na kwamba anajutia matendo yake. Mwanamume huyo alisema kila mja huhitaji kupewa fursa ya pili kutafakari maisha yake na kujirekebisha.

Alimsihi hakimu amfunge kifungo cha nje aendelee kuchumia familia yake changa.

“Mheshimiwa naomba fursa ya pili nitafakari kuhusu mustakabali wa maisha yangu na kuwa raia mwema. Nimekuwa gerezani tangu Desemba 7, 2020, na nimejifunza mengi. Nimekuwa na nafasi ya kumrudia Mungu na kutubu dhambi zangu nilizotenda kwa kuongozwa na tamaa. Nimejua sasa uhalifu haulipi na haufai,” Keverenge alisema huku akidondokwa na machozi.

Mshtakiwa alifichua kwamba akiwa gerezani, aliwapoteza jamaa wake wa karibu na hakuweza kupata fursa ya kuwazika na kutoa heshima zake za mwisho.

Hakimu aliamuru watano hao waendelee kukaa gerezani hadi Januari 29, 2024, atakapopewa ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia ya kila mmoja wao.

Washtakiwa walikuwa wamejishika tama walipokuwa kizimbani.

Endapo mahakama itakataa ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia, kila mmoja wa watano hao atasukumwa jela maisha.