Mchungaji aonya watoto wa Lizzie Wanyoike dhidi ya kupigania mabilioni yaliyoachwa
NA MWANGI MUIRURI
WATOTO watatu wa mwendazake Lizzie Muthoni Wanyoike mnamo Jumanne walionywa na wachungaji dhidi ya kupigania mabilioni ambayo wameachiwa.
Watoto hao ni Antony Wanyoike, Stella Njoroge na Eric Kariuki.
Bi Wanyoike aliaga dunia Januari 14, 2024 baada ya kuugua saratani ya mishipa ya uzazi yaani Fallopian tube cancer.
Wachungaji hao waliofika katika ibada ya mazishi ya mwekezaji huyo mashuhuri mwanzilishi wa Nairobi Institute of Technology and Business Studies na Mkahawa wa Emory walisema watabakia macho kuona jinsi watakavyorithi mali hiyo.
Makasisi hao wa kanisa la Kianglikana wakiongozwa na askofu Julius Njuguna wa Dayosisi ya Thika na mwenzake Joel Waweru wa Nairobi waliteta kwamba “yale tunayoshuhudia nchini ya watoto wakizozania mali iliyoachwa na wazazi ni ya kutamausha”.
Katika mahubiri yake, Askofu Waweru alionya watoto hao kwamba “mkianza kupigania hiyo mali mtakuwa mnatoa jasho la marehemu mama yenu kwa mawakili ambao watakamua pato lenu bila huruma kwa kisingizio cha kuwawakilisha mahakamani”.
Askofu Waweru alisema kwamba “sisi tutakuwa tunafuatilia vile mtaendeleza uwekezaji huu mkubwa wa mama yenu tukiwaombea muustawishe hata zaidi.”
Kando na taasisi hiyo ya Nairobi Institute of Technology and Business Studies, marehemu Wanyoike alikuwa pia mmiliki wa mkahawa wa Emory ulioko mtaani Kileleshwa jijini Nairobi.
Uwekezaji mwingine wa Bi Wanyoike ni shule za msingi na Sekondari, soko la hisa, Wakfu wa Lizzie Wanyoike na pia katika sekta ya nyumba.
Askofu Waweru aliwataka watoto hao kuzingatia maadili ya mama yao ambaye alisema “alipenda kusaidia wasiojiweza na pia kuwahami wengi na taaluma za kuwapa riziki”.
Aliwataka wajue kwamba “mama yenu hakuwa mbinafsi, mfisadi au mnafiki na moyo wake ulikuwa unafunguka kukumbatia wote bila ubaguzi”.
Aliwashauri watekeleze ushauri miongoni mwao “pasipo kuangalia nani mkubwa au mdogo kwa mwingine”.
Akasema “wewe Antony usiseme ni wewe mkubwa na uanze kukumbatia mali yote. Wewe nawe Stella usiseme eti wewe ndiye msichana wa kipekee…Eric nawe usiseme wewe kama mdogo unashikilia nafasi ya himaya hii”.
Aliwataka kukaa chini na kupanga vile wasifu wa Bi Wanyoike utaendelezwa kuwa wa kipekee nchini na uhifadhiwe kuwa kielelezo kwa vizazi.
Askofu Waweru aidha alisema ufisadi ulioko Kenya ni wa kushtua na usipokabiliwa, hakuna ustawi utawahi kuafikiwa.
“Hata Lizzie alikuwa ametudokezea vile baadhi ya maafisa wafisadi wa mamlaka ya ukusanyaji ushuru walimtembelea siku moja wakijaribu kumtapeli kwa hadaa na vitisho,” akasema.
Lakini Bi Wanyoike, akaongeza, “kwa kuwa alikuwa akilipa ushuru wake kwa njia ya uadilifu alikaa ngangari na akawaambia hangewapa hata ndururu na ilibidi waondoke wakiwa wamekunja mkia”.
Aliwashauri watoto hao wa Lizzie wajitahadhari na ujanja, ujeuri na udhalimu wa mafisadi na waelewe kwamba Bi Wanyoike alikuwa na marafiki wengi ambao watakuwa tayari kusaidia katika hali zote tata.