TAHARIRI: Tumsaidie Rais kumaliza ufisadi
NA MHARIRI
JUMATANO taifa zima liliadhimisha miaka 55 tangu kujinyakulia uhuru na kama kawaida rais alihutubia taifa na magavana nao wakahutubia kaunti zao mbalimbali. Ulikuwa wakati mwafaka wa kukumbuka wahanga wetu waliojitolea kukabiliana na makaburu ili kutwaa uhuru wa taifa hili.
Lenye uzito zaidi ni nguvu ya rais Kenyatta kukabili uozo wa ufisadi ambao unaonekana kutuzonga. Rais alitahadharisha wafisadi kwamba siku zao zimehesabika na kuwa watafagiliwa kwelikweli.
Matukio ya hivi majuzi yanaashiria kwamba kweli rais hacheki na mtu. Jana, rais alisema vita dhidi ya ufisadi vimeanza kuzaa matunda kwa kuwa maafisa wakuu serikalini waliodhani hawawezi kuguswa na yeyote tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi.
Aliwaonya pia watumishi wa serikali wanaotumia vibaya mamlaka, kwamba japo wanaweza kukimbia lakini hawatakuwa na pahala pa kujificha. Kwamba watalipa kila shilingi waliyopora.
Akihutubia taifa jana wakati wa maadhimisho ya miaka 55 tangu Kenya ijipatie uhuru, Rais alisema serikali yake imeanza mikakati ya kunasa walanguzi wa dawa za kulevya ambao matendo yao yamesababisha maafa makubwa kwa jamii. Rais anapaswa kushirikiana na mashirika ya kijasusi kutoka mataifa ya kigeni kama Interpol ili kunasa walanguzi wa watoto na dawa za kulevya.
Ni juu ya kila mmoja wetu kumsaidia Mheshimiwa Rais kuafiki malengo yake ambayo yatapelekea kutia nakshi utawala wake akiondoka 2022. Viongozi kutoka eneo la Bonde la Ufa, wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei wanapaswa kukoma kuingiza ukabila katika vita dhidi ya ufisadi. Wajue kwamba vita hivi havilengi watu wa jamii ya eneo hilo.
Madai yao kuwa vita hivyo vinanuia kutatiza ndoto ya naibu wa Rais William Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022 hayana mashiko kabisa.
Jitihada za rais katika kusaini mikataba na mataifa mbalimbali kama vile Uswizi, Uingereza na Kisiwa cha Jersey kuhakikisha fedha zilizofichwa katika nchi hizo na wafisadi zinarejeshwa nchini ni za kupigiwa mfano. Tumuunge rais katika vita dhidi ya ufisadi.
Idara ya Mahakama inayoongozwa na Jaji Mkuu David Maraga nayo pia isijikokote kushughulikia kesi za ufisadi nchini.