Wahanga wa Al-Shabaab warejelea mashamba yao baada ya kambi kufungwa
NA KALUME KAZUNGU
ZAIDI ya familia 200 za wakimbizi wa mashambulio ya Al-Shabaab Kaunti ya Lamu zimevunja kambi yao na kurudi vijijini mwao.
Hii ni kufuatia kuimarishwa kwa usalama kwenye vijiji vyao vilivyoko mashambani, ikiwemo kubuniwa kwa kambi za polisi.
Kambi ya wakimbizi ya Shule ya Msingi ya Juhudi, Lamu Magharibi, ilikuwa imebuniwa tangu Juni, 2023 kufuatia mauaji ya kila mara yaliyokuwa yakitekelezwa na Al-Shabaab kwenye vijiji vya Salama, Juhudi, Marafa na Widho.
Mapema juma hili, serikali kuu iliamrisha kambi hiyo ya wakimbizi kuvunjiliwa mbali na wakazi kurudi mashambani, ikishikilia kuwa usalama umedhibitiwa vilivyo.
Akizungumza na Taifa Leo Alhamisi, Mwenyekiti wa Maslahi ya Wakimbizi wa kambi ya shule ya Msingi ya Juhudi, Bw Joseph Ngige alisema kwa sasa kambi hiyo haipo tena kwani jumla ya familia 213 zilizokuwa zikiishi hapo zote zilitii amri ya serikali ya kuvunja kambi na kurudi kuishi vijijini mwao.
Bw Ngige aliishukuru serikali kuu kupitia kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kwa juhudi zake katika kuhakikisha wananchi na mali inalindwa vilivyo.
“Tunafurahia kurudi mashambani kwetu. Kambi imevunjwa kwa sasa. Tumewekewa kituo cha polisi hapa Salama. Wanajeshi wetu wa Ulinzi Kenya (KDF) pia wamekuwa wakipiga doria usiku na mchana kuhakikisha tuko salama. Kila kitu ki shwari kwa sasa,” akasema Bw Ngige.
Bi Pamela Ogutu, mkazi wa Salama, hakuficha furaha yake kufuatia hatua ya serikali ya kuboresha usalama na kuwarudisha wakimbizi vijijini mwao.
Bi Ogutu alishikilia kuwa angalau wanalala majumbani mwao usiku kucha kinyume na awali ambapo wangetembea mwendo mrefu hadi shuleni Juhudi kulala.
“Kuna wengine wetu tulikuwa tukilala msituni kila giza linapoingia kwa kuhofia kushambuliwa na Al-Shabaab. Twashukuru. Kujengwa kwa kituo cha polisi hapa Salama kumesaidia pakubwa kujenga imani yetu kuhusiana na usalama wa eneo hili,” akasema Bi Ogutu.
Bw Shadrack Njuguna, mkazi wa Juhudi, alisisitiza haja ya serikali kuwazingatia kwa kuwasambazia chakula cha msaada vijijini mwao, akichacha kuwa maisha baada ya kambini ni magumu.
“Ikumbukwe kuwa tulipoteza nyumba zetu zilizochomwa na Al-Shabaab wakati tukiwa kambini. Mimea yetu mashambani yote iliharibiwa na wanyama pori. Hakuna chakula hapa. Serikali itusaidie kuanzisha na kuendeleza maisha yetu baada ya kutoka kambini,” akasema Bw Njuguna.
Kati ya Juni na Septemba,2023, zaidi ya watu 30 waliuawa kwa kuchinjwa na Al-Shabaab ilhali nyumba zipatazo 40 na kanisa zikiteketezwa na magaidi wa Al-Shabaab kwenye vijiji vya Juhudi, Salama, Marafa, Widho na Poromoko, vyoke vikipatikana eneobunge la Lamu Magharibi.
Hatua hiyo ndiyo iliyosukuma kambi ya wakimbizi ya Juhudi Primary kubuniwa, ambapo wakazi wamekuwa wakikimbilia na kulala huko kila jioni na usiku kucha kabla ya kurudi makwao alfajiri.
Kambi hiyo imedumu kwa karibu miezi minane sasa kabla ya kuvunjwa juma hili.
Kuvunjwa kwa kambi hiyo kunajiri kufuatia juhudi za serikali kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Profesa Kithure Kindiki ambaye aliahidi kujenga kambi zaidi za walinda usalama na kusambaza walinda usalama kwenye vijiji vyote vya Lamu vinavyokumbwa na changamoto ya ugaidi.