Watu 11 wapoteza maisha katika ajali Ahero
NA CHARLES WASONGA
WATU 11 wanahofiwa kuaga dunia Jumatatu asubuhi baada ya basi la abiria aina ya Super Metro kugongana na lori katika eneo la Ahero katika barabara ya Kisumu-Nairobi.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Nyando Grace Thuo alisema waliojeruhiwa walikimbizwa hadi katika hospitali ya kaunti ndogo ya Ahero kwa matibabu.
“Gari hilo la abiria lilikuwa likielekea Nairobi na lori hilo lilikuwa likielekea upande wa Kisumu. Gari la tatu lililokuwa likifuatia gari hilo la Super Metro pia liliharibiwa,” akasema Bi Thuo.
Aliongeza kwamba jumla ya watu 53 walikimbizwa katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Ahero na hospitali nyingine za karibu.
“Waliopoteza maisha ni wanaume wanane, wanawake wawili na kijana mmoja,” akaeleza.
Duru zilisema kuwa ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa kumi na moja alfajiri na gari hilo la abiria lilikuwa likitoka Uganda likielekea jijini Nairobi.
Maiti za watu hao 11 zimehifadhiwa katika hifadhi ya hospitali ya kaunti ndogo ya Ahero huku mabaki ya magari hayo yakiburutwa hadi katika kituo cha polisi cha Ahero.
Eneo ambako ajali hiyo ilitokea lina sifa mbaya ya kushuhudia ajali kadha zinazohusisha malori na magari ya uchukuzi wa abiria.
Mnamo Oktoba 9, 2019, watu 15 waliangamia na wengine 35 wakajeruhiwa baada ya basi la abiria la kampuni ya Eldoret Express kugongana na lori la kubeba miwa katika mji wa Awasi, katika barabara hiyo ya Kisumu-Nairobi.