Habari Mseto

DPP kuchunguza uhusiano wa mlalamishi na mshtakiwa

January 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga amepewa muda kubaini uhusiano kati ya mfanyabiashara na afisa katika Ubalozi wa Brazil anayedai alitapeliwa Sh1.5 milioni katika kashfa ya kuuzia idara ya ulinzi (DoD) pombe ya makali.

Hii ni baada ya upande wa mashtaka kudai mshtakiwa na mlalamishi walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi lakini ukasambaratika.

Hatimaye Brian Birongo Motanya alikamatwa na kushtakiwa kwa kumlaghai Lydia Kemunto Magonga.

Aliposhtakiwa mwaka 2023, ilibidi Brian azungumze kwa Ekegusii mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina ili apewe dhamana kwa vile kulikuwa na tetesi kwamba hakuwa raia wa Kenya.

Ilibidi Seneta Okong’o Omogen amthibitishie hakimu kwamba Bw Birongo ni jirani yake na kwamba anawafahamu watu wao na kwamba anawafahamu wazazi wake.

Baada ya kupata thibitisho hilo, hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana.

Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi alimruhusu DPP muda wa kusoma na kubaini kupitia jumbe za WhatsApp na jumbe fupi ambazo Bw Birongo na Bi Kemunto walitumiana.

Bw Ekhubi alimpa muda DPP kusoma faili ya kurasa 340 za jumbe hizo ili abaini wawili hao walikuwa kwa uhusiano wa aina gani.

Hakimu huyo alimruhusu DPP kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Bi Virginia Kariuki kupekuapekua faili hiyo na kutenganisha ushahidi wote unaohusu ufisadi huo.

Bi Kemunto anadai kwamba alitapeliwa Sh1,520,000 na Bw Birongo katika kile anadai ni ufisadi kwa vile alielezwa watajumuika pamoja katika biashara ya kuuzia DoD pombe ya makali sawia na kuwekeza katika kilabu cha kuwahudumia mabwanyenye.

Bi Kemunto alidai kuwa alitapeliwa pesa hizo katika muda wa siku mbili kati ya Novemba 25 na Novemba 27, 2022, katika eneo la Westlands, Nairobi.

Katika kisa hicho cha kati ya Novemba 25-27, 2022 Bw Birongo inadaiwa alimweleza mlalamishi kwamba wangefanya biashara ya pamoja na kuuzia DoD pombe ya makali.

Mbali na kileo hicho, Bw Birongo inasemekana alimuahidi Bi Kemunto kwamba wangewekeza katika biashara ya kilabu ambacho kingewavutia mabwanyenye.

Mshtakiwa alikanusha kumtapeli afisa huyo wa ubalozi. Yuko nje kwa dhamana.

Kesi hiyo ilikuwa imeorodheshwa kusikilizwa Jumatatu lakini ikaahirishwa kwa vile ushahidi wa Whatsapp na SMS ulikabidhiwa kiongozi wa mashtaka Bi Kariuki na afisa anayechunguza kesi hiyo kortini.

Akasema Bw Ekhubi akiahirisha kesi: “Nimeona ukikabidhiwa faili ya kesi hii ukiwa hapa mahakamani. Wakili wa mshtakiwa anahitaji kupewa muda wa kujifahamisha na nakala hizo za jumbe za WhatsApp na SMS. Itabidi kesi hii iahirishwe hadi Mei 2024,” Bw Ekhubi alisema.