Habari Mseto

Mbunge afadhili wasichana waliojifungua kurejelea masomo

January 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA ERIC MATARA

WASICHANA 21 waliokatiza masomo baada ya kupata mimba Kaunti ya Kericho wamepata afueni kutokana na mpango maalum wa kuwawezesha kurejelea masomo katika shule mbalimbali eneo hilo.

Mpango huo uliozinduliwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kericho Beatrice Kemei utawanufaisha wasichana hao wenye umri kati ya miaka 18 na 26 waliokuwa wameacha shule baada ya kujifungua huku baadhi yao wakiolewa.

Mbunge huyo, kupitia mpango unaofahamika kama Mashujaa wa Elimu ya Mtoto wa Kike aliwatafuta na kuwapa fursa nyingine kupata elimu.

“Shule zilipofunguliwa muhula wa kwanza, kina mama wachanga waliokuwa wamekatiza elimu yao wasingerejea kwa sababu ya kukosa karo na mahitaji mengine,” Bi Kemei alieleza Taifa Leo.

“Nimewalipia karo na nitafadhili matumizi yao yote katika shule mbali mbali. Kina mama hao wachanga sasa wana nafasi ya pili ya kuendeleza elimu yao.”

Ivy Chepkoech,19, mama ya mtoto mmoja, ambaye ni miongoni mwa walionufaika na mpango huo, alikuwa mwingi wa shukran.

“Nimerejea shule kuendelea na elimu ya Kidato cha Tatu na nimejitolea kupata angalau alama ya B+ katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE). Namshukuru Bi Kemei kwa msaada wake na kamwe sitawahi kumsahau maishani mwangu,” alisema.