Habari Mseto

Nyong’o asifu mpango wa ujenzi wa SGR hadi Kisumu

January 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

GAVANA wa Kisumu Anyang’ Nyong’o, Jumanne amepokea kwa furaha tangazo la Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen kwamba serikali inapanga kupanua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) hadi jijini Kisumu.

Prof Nyong’o alitaja tangazo hilo kama habari njema, akiongeza kuwa mradi huo utaimarisha usafiri kati ya Kisumu na Uganda.

Alisema pia utarahisisha sana usafiri wa kawaida na usafirishaji bidhaa.

“Ningetaka kumshukuru Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen kwa kutangaza upanuzi wa reli ya SGR hadi Kisumu kuanzia mwaka huu,” akasema gavana huyo.

Prof Nyong’o pia alisema kuwa upanuzi wa reli hiyo utachangia ukuaji mkubwa wa bandari mpya ya Kisumu.

Alisema yamekuwa matamanio yao kwa muda mrefu kuhusu upanuzi wa mfumo wa usafiri kati ya eneo la Ziwa na maeneo mengine nchini.

“Tunatarajia hatua za haraka zitachukuliwa kuharakisha ujenzi wa mradi huu,” akasema.

Alisema kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wake, reli hiyo itachangia ukuaji wa kiuchumi katika eneo la Magharibi, kwa kulifungua eneo hilo kutembelewa na watalii, ikizingatiwa lina vivutio vingi.

“Ni jambo la kutia moyo sana kumsikia Bw Murkomen akitangaza serikali inapanga kumaliza angaa asilimia 35 ya mradi huo kufikia Desemba mwaka huu,” akasema.

Hapo awali, reli hiyo ilikuwa imepangiwa kujengwa kutoka Mombasa hadi Kisumu.

Hata hivyo, mradi huo, ulioanzishwa na serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, ulisimamishiwa jijini Nakuru kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha.

“Kama gavana wa Kisumu na mwenyekiti wa Jumuiya ya Kaunti za Eneo la Ziwa (LREB), ninaishukuru sana Serikali ya Kitaifa kwa kujitolewa kwake kupanua ujenzi wa SGR hadi Kisumu, na baadaye nchini Uganda,” akasema.