Arati awapa walimu wa chekechea mkataba wa Sh26,000 hadi Sh39,900 kila mwezi
NA WYCLIFFE NYABERI
WALIMU 714 wanaofunza chekechea (ECDE) katika Kaunti ya Kisii wamepata afueni baada ya serikali ya gatuzi hilo kuwapa ajira za kudumu.
Mishahara ya walimu hao pia imeongezwa kuliko waliyokuwa wakilipwa kabla ya kuajiriwa kwao kwa kudumu Gavana Simba Arati akijibidiisha kuinua viwango vya elimu Kisii.
Akizungumza mnamo Jumatano alipowapokeza walimu hao barua zao za kazi, mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini, alisema mchakato wa kuwahoji walimu hao ulizingatia nidhamu ya hali ya juu kutegemea na kufuzu kwa kila mmoja.
“Nina furaha kutangaza kwamba kulingana na sheria za uajiri, walimu waliochukuliwa wamewekwa katika vikundi mbalimbali vya kazi zenye mishahara ya kati ya Sh 26,000 hadi Sh 39,900,” gavana Arati alisema huku walimu hao wakimshangilia.
Bw Arati aliwashukuru walimu hao kwa kuonyesha uvumilivu, wakati walipokuwa katika harakati za kuwaajiri.
“Wakati wa kampeni zangu, niliahidi kwamba nikichukua wadhifa huu, nitazingatia masaibu yenu na leo tuko hapa,” Bw Arati aliongeza.
Gavana alithibitisha kujitolea kwake kuboresha ubora wa elimu ya ECDE na kuongeza kuwa ataendelea kuelekeza rasilimali zaidi katika ujenzi wa madarasa ya kisasa na miundomsingi yoyote inayohitajika.
Mapema Jumatano, Bw Arati alisimamia zoezi la kuzinduliwa kwa dawa za thamani ya zaidi ya Sh56 milioni kwa vituo mbalimbali vya afya katika kaunti hiyo.
Aliwaonya wahudumu wa afya na wafanyikazi wengine dhidi ya kuiba dawa za umma kwamba watakabiliwa na mkono wa ya sheria endapo watakamatwa.
Ili kuhakikisha matumizi ya dawa hizo ni ya busara, Bw Arati alisisitiza kwamba ni lazima rekodi zinazofaa zihifadhiwe ili iwe rahisi kuwasaka walio na tabia ya kusambaza dawa za umma katika maduka na hospitali za kibinafsi.
Ili kuimarisha utoaji wa huduma bora, Bw Arati alitangaza mipango ya kuwahamisha baadhi ya wahudumu wa afya kutoka kwa vituo vyao.