Mazishi ya mjakazi wa Khalwale yasimamishwa utata ukiibuka kuhusu alivyofariki
NA SHABAN MAKOKHA
KIZITO Amukune Moi, mwanamume anayedaiwa kuuawa na fahali wa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale hatazikwa Alhamisi Februari 1, 2024 kama ilivyopangwa.
Hii ni kutokana na utata mpya kuhusu chanzo haswa cha kifo chake huku wapelelezi wa DCI wakifanya uchunguzi zaidi.
Familia ilikuwa imepanga kuchukua mwili wa Kizito kutoka kwa chumba cha kuhifadhia maiti Jumatano lakini wakaambiwa wasifanye hivyo.
“Nilienda mochari saa kumi na moja unusu asubuhi kutayarisha mwili wa kakangu kabla wanafamilia wengine kuwasili. Lakini mwendo wa saa tatu asubuhi, nilipata simu kutoka nyumbani iliyoniambia kwamba polisi walikuwa nyumbani kusimamisha mazishi. Nilikimbia nyumbani nikakutana na maafisa hao walioniambia kwamba wana maagizo ya kusitisha mipango ya mazishi kwa sababu kulikuwa na utata,” akasema Fredrick Muhanji, kaka mkubwa na marehemu.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kakamega Kusini Benjamin Wambua alisema polisi walikuwa wamepokea malalamishi kutoka kwa umma ambayo yalihitaji kuchunguzwa.
Soma pia Khalwale afanya tambiko kwa fahali kumuua mfanyakazi
Halafu Mwaka mwingine wa Boni Khalwale bintiye akikwangura B+
Alisema hata hivyo kwamba familia ilikuwa imekwazika kwamba polisi hawakueleza ni nani haswa aliyewasilisha malalamishi hayo.
“Hata kama tumetii maagizo yao, bado tunauliza na tunataka kujua ni nani aliyeenda kwa polisi kutaka uchunguzi ufanyiwe mwili wa mwanangu,” akasema Bw Maurice Odanga Amukune, baba ya marehemu.
Bw Muhanji alisema familia ilikuwa imeshakubali ripoti ya upasuaji na kwamba hawakuwa na tashwishi yoyote kuhusu chanzo cha kifo cha jamaa yao.
“Tumelazimika kupunguza kasi ya mipango ya mazishi kwa uchunguzi zaidi baada ya madai ya mauaji kuibuka. Sasa tumeita maafisa wa kitengo cha jinai kufanya upasuaji mwingine kuondoa tashwishi yoyote kuhusu chanzo cha kifo chake,” Bw Wambua akasema.
Makachero wa DCI awali walikuwa wamehudhuria zoezi la upasuaji ambalo lilifanyika katika mochari ya Hospitali ya Kaunti ya Kakamega na lililotekelezwa na mpasuaji wa eneo la Magharibi Dickson Muchana, Jumatatu, siku moja baada ya mwili wa Amukune kupatikana katika zizi la ng’ombe nyumbani kwa Dkt Khalwale.
Bw Muhanji ambaye pia alihudhuria upasuaji huo alisema familia haina shaka kwamba kijana wao alifariki kutokana na majeraha yaliyosababishwa na fahali huyo.
Ripoti ilifichua kwamba Amukune alifariki kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya kudungwa na pembe za mfugo huyo.
Ripoti, aidha inasema kwamba mwendazake alikuwa na mbavu tatu zilizovunjika na majeraha katika shingo, kichwa na paja la kushoto.
Babake alisema mipango yote ya mazishi ilikuwa ishakamilika kwamba kijiji kizima cha Mungusi kilikuwa kimejiandaa kumpumzisha mwendazake.
Tulikuwa tushaandaa chakula cha kutosha kwa shughuli ya mazishi. Hata tulikuwa tumealika fahali wa kupigana kufika kwenye hafla. Jamaa na marafiki kutoka mbali pia wamewasili kwa ajili ya mazishi halafu washike shughuli zao. Huu upasuaji wa pili utatatiza ratiba za wengi,” akasema.
Kizito alikuwa keyateka wa fahali wa Seneta Khalwale. Inadaiwa alidungwa na pembe mpaka akafa na fahali aliyemtunza kwa miaka minne iliyopita. Alikuwa na umri wa miaka 46 na hakuwa na mke.
Dkt Khalwale alisema mila hutaka anayetunza fahali wa kupigana kuwa mtu ambaye hajaoa.
“Amukune alikuwa mwanamume mngwana ambaye angefanya kazi kokote, ila alichagua kuja kufanya kazi katika ulingo wa fahali wa mapigano. Tutaheshimu maagizo ya polisi na kusubiri mpaka wamalize uchunguzi wao ili kusiwe na tashwishi yoyote kuhusu alivyoaga dunia,” akasema.
Alishutumu wanasiasa wa Kakamega ambao anasema wameweka siasa katika suala la kifo hicho, jambo lililochelewesha mazishi.
“Hatua zote zinazohitajika kubaini chanzo cha kifo zimekamilika. Kile kinachoendelea kwa sasa ni siasa. Lakini sitapoteza muda kujibu propaganda na uvumi unaoenezwa mitandaoni. Hawa watu hawana utu kabisa kwa familia iliyoathiriwa,”alisema.
Fahali huyo aliyesababisha mauti alichinjwa na wanakijiji wenye ghadhabu kulingana na mila za Isukha na nyama ikagawanywa.
Bw Khalwale alikuwa wa kwanza kudunga mkuki kwenye shingo ya Inasio, ambaye alikuwa fahali kipenzi chake aliyeshinda mapigano mengi. Khalwale alimgombeza mnyama huyo akisema amemuaibisha.
“Inasio, umeniendea kinyume, umenikosea na kuniaibisha kwa kumfanyia visivyo mlezi na mkufunzi wako,” alifokea fahali huyo kabla ya kumchoma mkuki shingoni. Punde si punde, wanakijiji wakaishukia na kuanza kuikatakata vipande kabla hata iage dunia.
Bw Khalwale amenunua fahali mwingine atakayechinjwa wakati wa mazishi ya Amukune kumuenzi kwa huduma yake.