Habari Mseto

Kega ashauri Ruto kuwaweka kando washauri wake wa uchumi

February 1st, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, amewakosoa washauri wa Rais William Ruto kuhusu hali ya uchumi nchini, akisema “mashauri yao hayajaifaa nchi kukua kiuchumi”.

Mnamo Alhamisi, Bw Kega alisema kuwa Rais Ruto anafaa kushirikiana zaidi na mawaziri wake, badala ya kuzingatia mashauri yanayotolewa na washauri hao.

Baadhi ya washauri hao ni msomi wa masuala ya kiuchumi Dkt David Ndii (mwenyekiti), Dkt Nancy Laibuni, Dkt Augustine Cheruiyot, Bw Mohamed Hassan na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Adan Mohamed.

“Rais Ruto anafaa kuwaweka kando kwa muda washauri wake wa masuala ya kiuchumi na badala yake kushirikiana na mawaziri. Washauri hao ndiyo sababu kuu ambapo uchumi wa nchi unayumba,” akasema Bw Kega, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Kauli yake inajiri huku baadhi ya watu wakilaumu sera zinazoendeshwa na serikali ya Kenya Kwanza kutokana na kudorora kwa uchumi nchini.

Hata hivyo, baadhi ya washauri hao wamekuwa wakijitetea kwamba mashauri yao hayajakuwa yakizingatiwa na serikali.

“Huwa tunatoa mashauri yetu ijapokuwa huwa hayazingatiwi. Tutafanyaje?” akasema Dkt Ndii kwenye ujumbe mmojawapo alioandika mwaka 2023 katika mtandao wa X.

Bw Kega alisema kuwa kutokana hali mbaya ya uchumi nchini, thamani ya shilingi imeanza kushusha thamani yake dhidi ya shilingi za Uganda na Tanzania.

“Hapo awali, shilingi ya Kenya ilikuwa ikinunuliwa kwa karibu Sh30 za Uganda. Hata hivyo, thamani hiyo imeshuka hadi Sh23. Hali ni kama hiyo nchini Tanzania, ambapo shilingi moja ya Kenya inanunuliwa kwa Sh16 za Tanzania. Hilo ni ikilinganishwa na hapo awali, ambapo shilingi ya Kenya ilikuwa ikinunuliwa kwa Sh25 za Tanzania,” akasema.