Mamba aliyemla mtoto wa miaka 11 anaswa na kuuliwa
NA GEORGE ODIWUOR
MAAFISA wa Idara ya Huduma ya Wanyamapori (KWS) Ijumaa wamefaulu kumuua mamba aliyemla mtoto wa miaka 11 katika kijiji cha Manyuru, kaunti ndogo ya Ndhiwa.
Katika kisa hicho, mtoto huyo, Felix Odongo wa Gredi ya Pili alikuwa anachota maji na wenzake Mto Kuja wakati alipovamiwa na mamba huyo.
Mamake, Janet Auma alisema alikuwa nyumbani wakati mkasa huo ulipotokea.
“Nilitaka ale kwanza kabla kwenda mtoni lakini alisisitiza kwamba lazima amalize kazi za nyumbani kwanza kabla ya kula,” alihadithia Alhamisi.
Akiwa nyumbani, mama huyo anasema alisikia mayowe mtoni.
Mayowe hayo yalikuwa ya watoto wengine waliokuwa wanaita usaidizi kufuatia kunyakwa kwa mwenzao na mamba huyo.
Alipofika kwenye mto, Bi Auma anasema aliona mamba huyo akiogelea na kutoweka na mwanawe. Alikimbia kando kando ya mto kujaribu kumwokoa mtoto wake.
“Nilijawa na mshtuko usioelezeka nilipoona mamba huyo akiyoyomea majini na mwanangu,” alihadithia akiwa na majonzi mengi.
Wakazi hawakuwa na mbinu yoyote ila kusubiri maafisa wa KWS kuwasili kuwasaidia kumwinda mamba huyo.
Wakiwa wamejihami kwa mapanga na vifaa butu, wakazi walizunguka kwenye kingo za mto wakimtafuta mamba huyo huku ghadhabu zikigubika kijiji hicho.
Kufikia Ijumaa, ndio maafisa hao walifaulu kumpata baada ya majaribio kadhaa ya kumpiga risasi bila mafanikio awali.
Wakazi walifurika kumwona mamba huyo alipotolewa mtoni na huzuni ilijaa zaidi pale alipokatwa tumboni mwili wa mtoto huyo ukapatikana.
Mto Kuja ndio chanzo cha kutegemewa cha maji kwa wakazi wa Kabuoch, eneo la Ndhiwa na Sakwa Awendo, Kaunti ya Migori.
Chifu wa Lokesheni ya Kabuoch Magharibi Ann Anyango alisema mtu mwingine alikufa eneo hilo mwaka jana baada ya kushambuliwa na mamba huyo huyo, jambo linaloashiria hatari kubwa inayokabili wakazi wa eneo hilo.
Wengine wamejeruhiwa wakikimbia kujiokoa kutoka kwa meno ya mnyama huyo.
Bi Auma sasa anaomba wahisani wajitokeze wamsaidie kumzika mwanawe aliyekutwa na mkasa huo.
- Imetafsiriwa na Fatuma Bariki