• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kocha Mkenya aliyeenda mafunzo Arsenal ahitimu

Kocha Mkenya aliyeenda mafunzo Arsenal ahitimu

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Hamisi Mohamed amekamilisha mafunzo ya kipekee ya ukocha katika Shule ya Soka ya klabu ya Arsenal (Arsenal Soccer Schools) jijini London nchini Uingereza katika ziara yake ya wiki moja iliyoanza Desemba 7, 2018.

Kocha huyu almaarufu kama Coach Kaka hajaficha furaha yake ya kupata mafunzo hayo kutoka kwa mojawapo ya klabu tajika duniani kupitia ushirkiano wa kampuni ya kutoa huduma za kutuma na kupokea pesa ya WorldRemit na klabu ya Arsenal kutoka Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza.

“Imekuwa safari ya kufana sana. Kutazama mechi uwanjani Emirates ni kutimiza mojawapo ya ndoto zangu. Pia nimepokea mafunzo mengi muhimu. Naelekea nyumbani Kenya nikiwa na ujuzi mpya na mafunzo ambayo yatanisaidia kuimarisha mradi wangu na kazi ninayofanya katika shule ya kukuza talanta ya Young Talents. Nitakapofika Kenya, nitaandaa mafunzo ya makocha ili kuwapa ujuzi niliopokea. Ningependa kushukuru WorldRemit na Arsenal kwa fursa hii na natumai wataendelea na kazi hii nzuri ya kusaidia jamii,” alisema Mohamed.

Mkenya huyu alipata fursa ya kuzuru Arsenal baada ya kushinda makocha 700 kutoka Bara Afrika katika zoezi lililofikia kilele kuchagua kocha mmoja kutoka orodha ya makocha sita waliofika fainali. Kura yenyewe iliandaliwa kati ya Septemba 28 na Oktoba 5, 2018 na Mohamed akiibuka mshindi kwa zaidi ya aslimia 35.

Katika ziara yake ya London, Mohamed, ambaye ni mwanzilishi wa shule ya kukuza talanta ya Young Talents katika eneo la Embul Bul, Ngong’ katika kaunti ya Kajiado, alijifunza falsafa ya ukocha ambayo imesaidia Arsenal kuweka viwango vya juu katika soka na kupendwa kote ulimwenguni.

“Alikuwa na kipindi cha ana kwa ana na Kocha Mkuu wa shule ya soka ya Arsenal, Simon McManus. Pia alifurahia ziara ya kibinafsi katika uwanja wa Emirates na mapokezi ya VIP wakati wa mechi ya Ligi Kuu kati ya Arsenal na Huddersfield Town,” wadhamini wa safari hiyo WorldRemit, wamesema Alhamisi. Kampuni hiyo imeongeza pia ilifanya mipango ya Mohamed, ambaye kwa jina la utani ni Coach Kaka, kukutana na washauri na mashirika yaliyo na ushawishi mkubwa katika jamii ya Waafrika nchini Uingereza kumsaidia kupanua na kuendeleza miradi yake ya ukocha. M

apema juma hili, Mohamed alikutana na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Rwanda Eric Murangwa Eugene, ambaye alidakia Rayon Sports enzi zake, na Mkenya Lydia Tett Olet. Wawili hawa wanaishi nchini Uingereza. Murangwa alianzisha taasisi ya Isham inayotumia nguvu za spoti na hadithi kuleta amani katika jamii na kuvumiliana. Olet ni mwanzilishi wa shirika la Kenya in the Park, shirika kubwa linaloleta Wakenya wanaoishi Uingereza pamoja katika shughuli mbalimbali ikiwemo michezo.

Coach Kaka na Murangwa walijadiliana kuhusu malengo yao na ujuzi waliopata katika kutumia michezo kuleta pamoja jamii zilizotengana. Olet na Mohamed walijadiliana jinsi jamii ya Wakenya wanaoishi ughaibuni inaweza kusaidia mradi wake. Kocha huyo chipukizi pia alikutana na viongozi wakuu wa kampuni ya WorldRemit kuzungumzia changamoto za kuimarisha shirika.

Maafisa Andrew Stewart na McManus kutoka WorldRemit na Arsenal Soccer Schools mtawalia, waliridhishwa na Mohamed. Wamesema wanasubiri kuona matunda ya ziara ya Mkenya huyo nchini Uingereza.

Wamefichua kwamba pia wao wamejifunza mengi kutoka kwa Mohamed na wanaamini atafanikiwa katika jitihada zake. Akiwa London, Mohamed pia alipiga picha akizuru majirani, Chelsea. Alilipiwa kila kitu na WorldRemit kuzuru Uingereza kwa mafunzo hayo ya ukocha. WorldRemit ni wadhamini wa rasmi klabu ya Arsenal wa kutuma na kupokea fedha.

You can share this post!

Mama wa miaka 22 akana kumuua mwanawe

NAMIBIA: Jamii inayokaribisha wageni kwa ngono

adminleo