Habari za Kitaifa

Embakasi: Nema yatimua maafisa wanne kwa kutoa leseni tata

February 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

BODI ya Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema) imewatimua maafisa wanne kwa kutoa leseni kwa Maxxis Nairobi Energy.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nema Emilio Mugo alisema Jumamosi kwamba wamefikia uamuzi huo huku uchunguzi wa mlipuko wa gesi Embakasi ukiendelea.

Waliotupwa nje huku uchunguzi ukiendelea ni Mkurugenzi wa kitengo cha uzingatiaji wa masuala ya mazingira na kaimu naibu mkurugenzi. Wengine ni afisa wa mazingira wa ngazi ya juu – kitengo cha EIA, na mkuu wa kutathmini athari kwa mazingira – kitengo cha EIA .

Nema ilikubali kwamba ilipokea ripoti ya kimazingira kuhusu pendekezo na mpango wa ujenzi wa kituo hicho na Derdols Petroleum Limited huku jina la biashara likiwa Maxxis Nairobi Energy.

Nema ilisema ilipokea ripoti hiyo mnamo Julai 29 , 2020, na kuipa nambari NEMA/PR/5/223790 (PSR 16708).

Mamlaka ilisema iliorodhesha mradi huo kama wenye uwezekano wa kukumbwa na hatari katika kiwango cha kadri.

Ilieleza kuwa iliwaslisha ripoti hiyo kwa taasisi kadhaa za kutoa leseni zikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti Bei za Petroli na Mafuta (Epra), Mkurugenzi wa Mipango ya Ardhi katika Kaunti ya Nairobi, Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Maji (WRA), Idara ya Kusimamia Usalama kwenye Mijengo ya Ardhi (DCSH), Kampuni ya Kusimamia Maji ya Nairobi na Mkurugenzi wa Mipango ya Ustawishaji wa Miji.

“Baada ya kutathmini kwa kina mchakato wa kina wa mradi huo, Bodi ya Usimamizi wa NEMA imebaini mapungufu mengi kwenye utaratibu wa utoaji wa leseni yake kwenye kituo cha gesi husika. Bodi ilibaini kuwa maafisa wake wanne walihusika ambapo imetoa maagizo wakabiliwe kisheria,” Bw Mugo kwenye taarifa.

Alisema mamlaka hiyo imeziagiza taasisi husika za serikali kuanza mchakato wa kuwachukulia hatua maafisa hao.