Habari Mseto

Ajabu ya polisi wa Utawala kumnasua mwenzao mshukiwa wa wizi

December 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MANASE OTSIALO na HILLARY KIMUYU

MAAFISA wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Mandera Mjini waliachwa vinywa wazi baada ya polisi 14 wa Utawala waliokuwa wamejihami kujitoma ndani ya kituo hicho na kumwokoa mmoja wao ambaye alikuwa amezuiliwa kwa seli.

Polisi hao wa Utawala kutoka kitego cha RDU Mandera, kambi ya Kapendo waliingia kituoni humo huku wamevalia sare kamili za vita na kujihami na bunduki aina ya G3 saa mbili unusu asubuhi.

Walipiga risasi hewani huku maafisa wanne wakitaka wapewe funguo za seli za wafungwa akitisha kupiga polisi wa kituoni risasi.

“Wengine walisalia kulinda doria lakini mmoja kati ya wanne aliyekuwa kwa deski alielekeza bunduki yake kwa maafisa wetu akitaka funguo za seli,” akasimulia mmoja wa maafisa aliyehojiwa na Taifa Leo.

Walifululiza na kufungua seli za mahabusu wanaume na kumchukua mfungwa mmoja, aliyetambuliwa kama Richard Githaka Karanja, aliyekamatwa kwa madai ya wizi wa mabavu mjini Mandera..

Mshukiwa huyo aliyetoka kwa seli akitabasamu, alikuwa afikishwe mahakamani jana asubuhi kujibu mashtaka.

Ndani ya seli, kuliwa na wafungwa 12 lakini hakuna aliyetoroka wakati wa kisa hicho kilichochukua dakika tatu pekee.

Maafisa wa RDU walipiga risasi hewani mara nne na kumwondoa mwenzao na kuondoka wakielekea kambi yao ya Kapendo, iliyoko kilomita tano kutoka kituo hicho.

Wakiondoka, waliapa kuwa kamwe hawawezi kuwaruhusu polisi wa kituoni kumzuilia mmoja wao.

Hakuna yeyote aliyepata majeraha wakati wa kisa hicho. Waliokuwemo katika kituo hicho ni OCS, walinzi wawili wa kituo, polisi wasimamizi, polisi wa kituoni, walinzi wa seli na mwelekezi.

Polisi wamekuwa wakichunguza kisa cha wizi wa mabavu katika kituo cha mafuta cha Takbir, mjini Mandera ambapo mlinzi aliuawa na Sh700,000 kuibwa.

Genge la wezi saba liliingia kwa kituo hicho huku limevalia sare za polisi, kulingana na mlinzi ambaye alinusurika katika uvamizi huo.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mandera Lawrence Omondi alithibitisha kuwa kulikuwa na uvamizi katika kituo hicho cha polisi, lakini akajiepusha na kutoa taarifa zaidi.