Habari Mseto

Chapati zapikwa kwa unga ngano uliokandwa kwa miguu

February 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MAOSI

HALI ya hatari inawakodolea macho Wakenya, ikifichuka kuwa baadhi ya wapishi katika vibanda na hoteli  za mitaani, hukanda unga wa ngano wakitumia miguu peku.

Hii inaleta hofu ya mkurupuko wa maradhi kwenye mikahawa ya vichochoroni na kwenye mitaa ya mabanda ambayo baadhi ya watu hawaweki zingatio kwa usafi wa hali ya juu.

Asilimia kubwa ya wapishi wanaoendesha biashara za kupika chakula nyakati za usiku wanaendelea kumulikwa kwamba huwa ba mazoea ya kukanda unga kwa miguu.

Taifa Leo ilikutana na muuzaji chapati ambaye tunamuita *Sharon. Yeye anasema kwamba hili ni jambo la kawaida katika mikahawa mingi wala sio jambo ambalo lilianza juzi.

“Tumekuwa tukikanda unga wa ngano kwa miguu bila kuvalia chochote miguuni,” akasema * Sharon.

Naye mmoja wa wamiliki wa mikahawa ya vyakula eneo la Pipeline, Nairobi anasema wakitumia mbinu hiyo, inawachukua muda mfupi kuandaa mapochopocho na pia hupunguza gharama ya kuajiri wapishi.

Kwanza ni njia maarufu ambayo hutumika na wapishi wanaohudumia idadi kubwa ya wateja.

Anasema kabla ya kufungua kazi yake, alijifunza kukanda unga kwa kutumia miguu kutoka kwa mwajiri wake wa awali.

Mwanzoni alikuwa akishangaa ni kwa nini mhudumu wake alikuwa akipokea idadi kubwa ya wateja.

Alichukulia kama ni mzaha ila baadaye alikuja kubaini kwamba unga unapokandwa kwa miguu, hutengeneza chapati laini.

Lakini anapuuzilia mbali madai kwamba chapati hizo zina athari mbaya kiafya, akisema viini vyovyote huchomwa na mafuta moto.

Anasema wateja wengi jijini Nairobi hawajui chapati na mandazi wanayokula na kufurahia kila siku huandaliwa namna gani.

Ni shughuli ambayo huendeshwa kwa siri kubwa ingawa baadhi ya wamiliki na wateja wamewahi kusikia au kushuhudia visa kama hivi.

Hii ikiashiria kwamba inahatarisha afya ya umma hususan kwa wateja wasiokuwa na habari.