Habari Mseto

Mkiweka kapu moja la kukusanya ushuru hamtalia pesa sana, magavana waambiwa

February 10th, 2024 1 min read

GEORGE ODIWUOR NA WANDERI KAMAU

SERIKALI ya kitaifa inazitaka serikali za kaunti kuwekeza kwenye mifumo ya kidijitali ya kukusanyia mapato, kama njia moja ya kusuluhisha changamoto za kifedha zinazozikumba kaunti.

Mnamo Ijumaa, Katibu wa Ugatuzi, Bi Teresia Mbaika, alisema kuwa serikali za kaunti zina uwezo wa kuzalisha mapato yake na kuyatumia kushughulikia baadhi ya mahitaji yake.

Hata hivyo, aliwaambia magavana kukumbatia njia za kidijitali za kukusanyia fedha, alizozitaja kuwa bora zaidi kwenye ukusanyaji wa mapato.

Mifumo ya kidijitali inahusu matumizi ya simu za mkononi.

Mifumo hiyo huwa inazuia fedha kupotea, kwani huwa zinaelekezwa katika eneo moja.

Fedha nyingi ambazo huwa zinakusanywa na maafisa wa kaunti kutoka kwa wafanyabiashara na wahudumu wengine huwa hazizifikii kaunti, kwani nyingi huwa zinaporwa na maafisa hao.

Magavana wengi wamekuwa wakilalamikia ucheleweshaji wa fedha kutoka kwa serikali ya kitaifa, hali ambayo imekuwa ikichangia migomo, ucheleweshaji kwenye utoaji wa huduma kwa umma kati ya matatizo mengine.

Bi Mbaika alisema kuwa kaunti nyingi zina uwezo wa kuzalisha fedha za kutosha kuendesha shughuli na mipango yake.

Aliwashauri magavana kuzuru katika kaunti nyingine ili kuelewa sababu ambapo baadhi ya kaunti zinafanya vizuri kuliko nyingine kwenye ukusanyji fedha.

“Tunawapongeza magavana kwa kazi nzuri wanayofanya. Kutumia mfumo wa kidijitali kwenye ukusanyaji mapato kutaisaidia serikali kwenye utoaji wa huduma kwa raia,” akasema.

Bi Mbaika alikuwa akihutubu katika Kaunti ya Homa Bay, Ijumaa, chini ya mwaliko wa Gavana Gladys Wanga.

Homa Bay ni miongoni mwa kaunti zinazoongoza kwenye ukusanyji wa mapato kupitia mfumo wa kidijitali.

Katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022, kaunti hiyo ilikusanya jumla ya Sh318 milioni.

Hata hivyo, kiwango hicho kimeongezeka na kufikia Sh674 milioni kufikia Julai mwaka uliopita.

Mnamo Januari, kaunti ilikusanya jumla ya Sh108.3 milioni.

Serikali imekuwa ikisisitiza kuhusu umuhimu wa matumizi ya mfumo wa e-Citizen kwenye ukusanyaji fedha ili kuboresha mapato na kupunguza visa vya ufisadi.