Safari ya Lowassa kuanzia kuzaliwa hadi kuwania urais
NA MWANANCHI
MWANASIASA Edward Lowassa ambaye aliaga dunia Jumamosi baada ya kuugua magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu, ni mfano wa mtu aliyeanzia chini hadi kukwea ngazi ya juu katika uongozi wakati wa uhai wake.
Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953, katika kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.
Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967. Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa Kidato cha Kwanza mpaka Kidato cha Nne kati ya mwaka 1968 – 1971, kabla ya kumalizia Kidato cha Tano na Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu kwa kutuzwa Shahada ya Sanaa katika Elimu na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa afisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa alimuoa Regina Lowassa na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert, na Richard.
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3.
Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umaskini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mifugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dkt Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa Wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu, huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu mkubwa.
Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya wake ni u-waziri mkuu na sio kingine…”
Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote.
Lowassa ni miongoni mwa wana-CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa.
Mnamo Oktoba 2015, Lowassa aligombea urais kupitia tiketi ya vyama vya upinzani chini ya mwavuli wa Ukawa lakini akabwagwa na John Magufuli.
Tume ya uchaguzi nchini Tanzania ilitangaza kwamba Dkt Magufuli alizoa asilimia 58 ya kura huku mpinzani wake mkuu–Lowassa–akizoa asilimia 40 ya kura halali zilizohesabiwa.
Lowassa alipinga vikali matokeo hayo ambapo awali alikuwa ametoa madai kwamba alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 62 ya kura.
Soma Pia: Tanzia: Mwanasiasa mkongwe Edward Lowassa aaga dunia