Makala

KANSA: Wakenya wahamasishwa kuhusu gonjwa hatari Nairobi

December 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

NA PETER MBURU

ENDAPO watu wangefahamu uchungu mwingi wanaopitia wagonjwa wa saratani, huenda wangefanya juu chini kujiepusha na tabia na hali ya maisha ambayo inazidisha uwezekano wa kuugua ugonjwa huo.

Hii ni ikizingatiwa takwimu za kitaifa kuhusu ugonjwa huo, ambazo zinaonyesha kuwa unazidi kusambaa nchini na kuaThiri watu wengi kuliko mbeleni, vifo vinavyotokana nao vikizidi kuongezeka.

Mara nyingi ni vigumu kwa wagonjwa wa saratani ama watu wasiougua kutangamana na wataalamu kushauriwa kuhusu njia salama za kujiepusha na ugonjwa huo, ama hata watu ambao wamewahi kuugua kuelezea kuhusu hali anayopitia mgonjwa wa saratani.

Lakini Ijumaa, kikundi cha vijana wanaojiita The Future Foundation kiliandaa kongamano katika hoteli ya The Luke Jijini Nairobi, ambapo wataalamu kuhusu ugonjwa wa saratani, watafiti, wagonjwa pamoja na wadau wengine walielimishwa kuhusu ugonjwa huo hatari.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kenyatta apokezwa cheti cha mafunzo na mwenyekiti wa shirika la The Future Foundation katika hoteli ya The Luke, jijini Nairobi Desemba 14, 2018. Picha/ Peter Mburu

Mienendo ya watu

Katika kongamano hilo, iliibuka kuwa kuna tabia nyingi wanazofanya watu ambazo mwishowe zinaishia kuwa kiini kinachosababisha ugonjwa wa saratani, wakishauriwa kujizoesha kuishi maisha ya hali salama kiafya.

“Kikundi chetu ni cha kusaidia jamii, tumekuwa tukiwatunza mayatima, kuwezesha watu na kusaidia vijana kwa michezo, mazingira na mambo ya afya,” akasema Bw Mugo Wa Maina, kiongozi wa The Future Generation.

“Tulikuja baada ya kuona kuwa watu wetu wanaangamia kwa sababu ya saratani na tunafahamu kuwa makali ya ugonjwa huo yanaweza kupunguzwa ikiwa utatambuliwa mapema. Hiyo ndiyo maana leo tumeita watu wenye utaalamu kuhusu mambo ya saratani watueleze kuhusu ugonjwa huu na kile tunaweza kufanya ili kujiepusha nao, ama kusaidia wale ambao tayari wameugua,” akasema.

Na kwa hatua hiyo, kikundi hicho kilitoa nafasi kwa watu waliohudhuria kufunzwa na wataalamu, akiwamo mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, pamoja na watu ambao wamepitia uchungu wa ugonjwa huo.

Bi Sally Agallo ambaye ana miaka 48 alieleza Taifa Leo uchungu ambao alipitia wakati alipokuwa akiugua saratani kwa takriban miaka kumi.

Bi Sally Agallo aliyepona maradhi ya saratani. Picha/ Peter Mburu

Kansa ya sehemu tofauti

Japo kwa bahati nzuri mama huyo alithibitishwa kupona miaka mitatu iliyopita, matatizo aliyopitia wakati huo bado yapo hadi leo hii, kila mara akitaka kuzungumzia watu ili wajue umuhimu wa kupimwa, ili ikiwa mtu ana ugonjwa huo utambuliwe mapema na apatiwe tiba. Bi Agallo aliugua mara tatu, tena saratani za sehemu tofauti.

“Kuanzia mwaka wa 2007 nilipatikana na ugonjwa wa saratani ya uzazi na nikafanyiwa upasuaji ambao ulifanikiwa na baadaye ikapona. Baada ya miaka mitatu, tena nilipatikana na saratani ya koloni,” Bi Agallo akaeleza Taifa Leo.

Alisema hata baada ya kutibiwa na kupona kansa hiyo ya pili, bado alipatikana na nyingine ya njia ya choo, katika safari ya uchungu uliompiga mwongo mzima.

“Kwa sasa nashukuru kwa maana nilipona na sipokei matibabu tena na ndio maana nimejitolea kuhamasisha watu kwa jamii kuwa ni muhimu mtu kupimwa kwa kuwa ni hapo ambapo niliweza kujua mapema na nikatibiwa.

“Watu wasiogope wala kudhani kuwa kupatikana na saratani ni kifo. Pia ni vyema watu kujiunga na watu wanaougua kwa ajili ya kutiana moyo,” Bi Agallo akasema.

Bi Sally Agallo aliyepona maradhi ya saratani aonyesha kifaa cha matibabu ya ugonwja huo. Inamgharimu mgonjwa Sh1,000 kila siku kukinunua kwa matumizi. Picha/ Peter Mburu

Changamoto za kifedha

Alieleza kuhusu matatizo ya kifedha ambayo wagonjwa wa kansa hukumbana nayo.

“Saratani iko na gharama sana, wagonjwa wa saratani wanapitia mambo magumu sana kimatibabu. Hakuna mgonjwa nimezungumza naye akaniambia alitumia chini ya Sh1 milioni kwa matibabu, na wengi hutumia zaidi ya kiwango hicho.”

Kulingana na Bw Raphael Kinuthia, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, watu wanaougua ugonjwa huo wanazidi kuongezeka kadri muda unavyosonga, kutokana na hali ya watu kubadili maisha na kuwa na hulka ya kukosesha mwili mazoezi.

“Saratani ni mojawapo ya magonjwa yaliyosambaa sana ambayo si ya kuambukizwa. Baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa huu ni hali ya maisha ya watu kama uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, kukosa mazoezi ya mwili, ulaji wa vyakula visivyo salama na kuvuta hewa chafu,” akasema Bw Kinuthia, ambaye pia ni mtaalam wa magonjwa ya mwili.

Mwenyekiti wa shirika la The Future Foundation katika hoteli ya The Luke, jijini Nairobi Desemba 14, 2018 akihojiwa na Taifa Leo Dijitali. Picha/ Peter Mburu

“Mtu anapojua baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuzidisha uwezekano wa kupata kansa anaweza kuepuka,” akasema

Alisema kuwa nchini Kenya, wanawake wanawazidi wanaume kwa kuugua ugonjwa huo.

“Kulingana na takwimu za kitaifa kuhusu ugonjwa wa saratani, wanawake wengi huugua saratani ya matiti na sehemu ya uzazi kwa asilimia 40, huku wanaume wakiugua zaidi saratani ya koromeo na sehemu ya uzazi ambazo zinajumuisha asilimia 20. Kijumla, saratani za wanawake zinaongoza, japo hata watoto pia watoto wanaugua. Kuna ongezeko la watu kuugua saratani nchini,” akasema.