Jinsi wahamiaji kutoka mashambani wachangia mzigo wa basari mjini
NA SAMMY KIMATU
UHAMIAJI wa watu jijini Nairobi kutoka maeneo ya mashambani kwa ajili ya kusaka ajira unachangia ongezeko la hitaji la pesa kugharamia karo miongoni mwa wakazi mitaani ya mabanda.
Akiongoza hafla ya kugawa fomu za basari katika wodi ya Landi Mawe, Msaidizi wa Binafsi, Bw Stephen Okwach Isa aliyewakilisha Mwakilishi wa Wadi, Bw Simon Maina Miche, aliambia Taifa Leo wanafunzi 400 watapata basari zao wakati wowote mwezi huu.
Aidha, Bw Isa aliongeza kwamba waliokosa kufanikiwa kupata basari muhula huu wamehakikishiwa nafasi katika muhula ujao.
“Sisi hatuwabagui wakazi wa Landi Mawe. Tunaanza na wanaoishi na ulemavu kisha walio na viwango vya juu vya umaskini miongoni mwa masuala mengine. Tunachukua majina ya wale hawajapata leo ndiposa tutangulize basari zijazo na kundi hili,” Bw Isa akasema.
Vilevile, kupitia kwa Wakfu wa Simon Maina, familia zaidi ya 100 hufaidika katika mradi wa Chakula cha Mgao katika kila kipindi cha mara moja kwa kila miezi mitatu kila mwaka.
Kadhalika, aliongeza kwamba asilimia zaidi ya 90 ya wakazi mitaani ya mabanda wanaoishi ndani ya Wadi ya Landi Mawe ni walala hoi ambao kupata mlo na kusomesha watoto ni mzigo kwao.
“Wengi wao hufanya kazi za sulubu hasa wamama kwa kufua nguo huku wanaume wakibahatisha kupata vibarua vya mijengo na kibarua katika Eneo la Viwanda,” Bw Isa asema.
Hali hiyo, aliongeza, ilichangiwa na watu wengi kuwachishwa kazi Viwandani baada ya ujio wa corona.