Wakazi wakimbilia hospitali kusaka matibabu pombe ikiua tena
Na STANLEY NGOTHO
WATU wawili wameripotiwa kufa mjini Kitengela, Kajiado Mashariki, baada ya kunywa pombe haramu Alhamisi jioni.
Vifo hivyo vya ghafla vimesababisha taharuki katika eneo hilo lenye wakazi wengi huku watu kadhaa wakikimbia vituo mbalimbali vya matibabu kufanyiwa vipimo wakihofia kupoteza maisha yao.
Wahasiriwa hao wawili waliaga dunia katikia Hospitali ya Kitengela mnamo Ijumaa na Jumamosi mtawalia.
Stakabadhi za hospitali zilizoonwa na Taifa Leo zinaashiria kuwa Bw Dominic Muna,41, aliyeaga dunia akitibiwa, alipelekwa kituo hicho na marafiki Ijumaa jioni akiwa hali mahututi baada ya kupofuka.
Mnamo Jumamosi jioni, tulikutana na mama na jamaa zake mhasiriwa katika Hospitali ya Kitengela ambapo waliutambua mwili wake.
“Tunachofahamu tu ni kwamba alikunywa pombe haramu katika eneo la Panai Alhamisi jioni. Alikuwa muuzaji wa mayai kwa bei ya jumla mjini Kitengela. Inasikitisha mno kuwa watu wetu wanauawa na pombe haramu huku serikali ikitazama,” alisema jamaa wa familia hiyo.
Bw Peter Muturi, 52, mhasiriwa wa pili, alifariki dunia katika hospitali hiyo, kitengo cha dharura, Jumamosi usiku mwendo wa saa nne kasoro dakika ishirini.
Alikimbizwa katika kituo hicho baada ya kupofuka na hali yake kuzorota zaidi huku mke akijitahidi kuchangisha Sh5,500 za kununua dawa, alizoandikiwa na usimamizi was hospitali, katika duka la kuuzia dawa.
Juhudi za kumhamisha katika kituo kikubwa zaidi ziliambulia patupu kwa kuwa ambulensi ya hospitali ilisemekana kuwa na hitilafu huku mkewe mhasiriwa akishindwa kupata hela za kulipia ambulensi ya kibinafsi.
Haya yamejiri siku chache tu baada ya watu wasiopungua 13 kuaga dunia na wengine kupofuka kutokana kubugia pombe haramu katika Kaunti ya Kirinyaga.