Habari Mseto

Mafunzo kwa waendeshaji maboti, ukaguzi kutumika kuimarisha usalama baharini

February 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WACHIRA MWANGI

MAMLAKA ya Usafiri wa Baharini (KMA) itaanza usajili na ukaguzi wa meli zote zinazohudumu katika Bahari Hindi na maji ya maziwa bila malipo kuanzia Aprili 1, 2024.

Kulingana na Waziri wa Madini na Masuala ya Uchumi wa Baharini Salim Mvurya, meli hizo zitakuwa na nambari za utambulisho za kipekee kama sehemu ya kuhakikisha kuwa zinafanya kazi katika mazingira salama ili kuruhusu waendeshaji zaidi kusajili meli zao na vyombo vingine vya majini.

“Tumetoa msamaha wa kufanya hivi bure ili kuhakikisha kuwa wanastahili baharini na wanaafikia vigezo vya msingi vya usalama ili kudhibiti shughuli za uokoaji,” waziri Mvurya alisema.

Akizungumza kwenye hafla ya kuapishwa kwa Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa Bandari Maritime Academy (BMA) Eric Katana Lewa jijini Mombasa, Bw Mvurya alisema KMA na mashirika mengine ya serikali ikiwa ni pamoja na Kenya Coast Guard Service, Bandari Maritime Academy, na serikali za kaunti ziko tayari kuzindua programu ya mafunzo ya waendeshaji maboti kuanzia Machi 1, 2024.

“Nina furaha kutangaza kwamba hadi sasa tumeweza kutoa mafunzo kwa waendeshaji wa mashua 5,410 na watahamia kwa maziwa nchini kuanzia Machi ili kuwafunza wengine,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali imeanza mafunzo kote nchini ili kuimarisha utendakazi salama wa meli kulingana na agizo la Rais William Ruto kuimarisha usalama katika maji ya Kenya.

Mafunzo hayo yanawalenga waendeshaji maboti, wavuvi, Vitengo vya Usimamizi wa Ufukwe (BMUs) katika Bahari ya Hindi na maji ya ziwani; masuala ya uendeshaji wa maboti ya kisasa, taratibu za usalama wa baharini, ujuzi wa vitendo katika uendeshaji wa vyombo na ujuzi wa kiufundi ambapo pia wanafanyishwa mitihani.

KMA ilisema kuwa kuna waendeshaji wengi wa maboti na meli walio na uzoefu wa kimsingi wa kuendesha vyombo hivyo lakini hawana uthibitisho na stakabadhi zinazohitajika.

“Mafunzo hayo yatawawezesha waendeshaji kupata cheti kinachohitajika kuendesha meli kwa usalama na kufuata kanuni za baharini nchini,” Mwenyekiti wa KMA Hamisi Mwaguya aliambia Taifa Leo.

Kuhusu Mafunzo ya STCW, waziri Mvurya alitangaza kwamba KMA na BMA katika muda wa wiki mbili zijazo, wanakadiria kupunguza ada kwa ajili ya Mafunzo ya Kimataifa ya Viwango vya Mafunzo, Vyeti na Utunzaji wa Mabaharia (STCW) ambayo kwa sasa ni Sh35,000.

“Kumekuwa na mijadala mingi kutoka kwa vijana na viongozi kwamba mafunzo ni ghali. BMA tayari imepunguza ada za mafunzo ya kitaaluma ya mwendeshaji wa mashua kutoka Sh125,000 hadi Sh70,000,” Bw Mvurya alisema.

Kuhusu kuajiri Wakenya kufanya kazi nje ya nchi, waziri alisema kuwa KMA na BMA zitashirikiana na taasisi nyingine ili kuwe na uwiano katika kuajiri na kuwafunza wanaojisajili kupokea mafunzo.

[email protected]