Habari Mseto

Mbinu za kukabili harufu mdomoni kwa walio na uvundo licha ya kupiga mswaki

February 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA PAULINE ONGAJI

Kuna baadhi ya watu ambao hukumbwa na shida ya kutoa harufu mbaya mdomoni licha ya kupiga mswaki kila siku, na kufuata taratibu zifaazo ili kudumisha usafi.

Kando na masuala ya kiafya, shida hii yaweza kusababishwa na vyakula tunavyokula kila siku. Kwa mfano:

Kitunguu na kitunguu saumu

Vyakula hivi vina viungo vya salfuriki (sulfuric) ambavyo hufyonzwa kwenye damu na kuingia mapafuni, kabla ya kupenyeza mdomoni kwa haraka. Lakini hii haipaswi kuwa sababu ya kujiepusha na mboga hizi kwani zina umuhimu wake. Hata hivyo, unashauriwa kupunguza matumizi.

Maziwa

Japo yana manufaa mwilini, maziwa huchafua kinywa ambapo bakteria kwenye ulimi hula asidi aina na amino (amuno acid) zinazopatikana kwenye maziwa na bidhaa zake, na hivyo kusababisha harufu mbaya mdomoni.

Kuna baadhi ya vyakula ambavyo kwa upande mwingine vinazuia harufuu mbaya mdomoni kama vile:

Mboga na matunda mabichi

Mboga na matunda kama vile pea, karoti na tufaha husaidia kuzalisha mate mdomoni na hii hupelekea kusafisha bakteria inayosababisha harufu mbaya mdomoni.

Aidha, mboga na matunda haya yana viwango vya juu vya nyuzi na hivyo husaidia kuondoa uchafu kwenye meno unavyoendelea kula.

Tikitimaji na matunda jamii ya chungwa

Matunda haya yana viwango vya juu vya virutubisho vya vitamini C ambavyo husaidia kuzuia maradhi ya kinywa kama vile halitosis inayosababisha maradhi ya gingivitis.

Tangawizi

Kiungo hiki kina kiungo maalum kiitwacho 6-gingerol ambacho huchochea uzalishaji wa kimeng’enyo maalum kwenye mate ambacho huvunjavunja salfa (sulfur) kinywani.

Jaribu kuchanganya tangawizi iliyogongwa, juisi ya ndimu na maji moto kisha usuuze kinywani.

Chai ya kijani

Tafiti zimeonyesha kwamba catechins na kemikali asili za kusafisha mwili zinazopatikana kwa wingi kwenye chai ya kijani zaweza saidia kukabiliana na tatizo la harufu mbaya mdomoni.

Maji

Unapokunywa maji kwa wingi basi unasafisha chembechembe za chakula mdomoni na seli zilizoangamia, na hivyo kufanya mdomo wako usiwe mazingira mwafaka ya kuzalisha bakteria zinazosababisha harufu mbaya mdomoni.