Wafugaji samaki wageukia kamera za CCTV kwa ulinzi
Na ANGELINE OCHIENG
WAFUGAJI wa samaki katika Kaunti ya Kisumu wamegeukia teknolojia maalum ya kamera za CCTV ili kulinda vidimbwi vyao vya kufugia samaki karibu na fuo.
Haya yamejiri huku kero ya wizi wa samaki ikizidi kuhangaisha wafugaji wa samaki na baadhi yao kukadiria hasara kuu. Kwa muda mrefu, wafugaji wamekuwa wakitegemea maafisa wa doria wa Kikosi cha Kusimamia Fuo (BMU) usiku katika upande wa ziwani.
Katika kisa cha hivi majuzi kilichorekodiwa mwaka uliopita, mmiliki wa shamba la kufugia samaki alipoteza samaki wakubwa zaidi ya 1,200.
Ili kuwapa afueni wafugaji samaki, Kampuni ya Aquaculture Barn, Kisumu ilizindua tekolojia maalum ya CCTV ili kulinda samaki wa kufugwa, miezi minne iliyopita.
“Tuligeukia kamera za CCTV ili tulinde vidimbwi vyetu, tunaweza pia kuzungumza na timu yetu kamera zinapowashwa na hata kumfukuza mwizi kwa kuzungumza naye,” anasema Mkurugenzi wa Aqua Barn,Vincent Odiwuor.