Habari Mseto

Hofu baada ya ajuza kubakwa na kuuawa

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na STEVE NJUGUNA

WAKAZI wa mtaa wa mabanda wa Maina, mjini Nyahururu, kaunti ya Laikipia Jumapili walipigwa na butwaa baada nyanya wa miaka 70 kubakwa na kuuawa kikatili katika eneo hilo.

Hisia ziliwazidia wakazi na jamaa baada ya polisi kufika eneo la tukio kuuchukua mwili wa mwathiriwa, aliyetambuliwa kama Margaret Wanjeri. Haikubainika mara moja waliotekeleza unyama huo.

Mwanamke huyo aliishi peke yake na alikuwa muuzaji wa kuni. Alinyongwa na kubakwa kabla ya mshambuliaji huyo kutoroka.

Kisa hicho cha mauaji ni cha tatu kuripotiwa katika eneo hilo katika muda wa miezi miwili. Kwenye visa vya awali, wanawake wawili walipatikana wameuawa katika hali ya kutatanisha .

Bi Purity Wangari, ambaye ni jirani wa mwathiriwa, alisema kuwa walishuku kwamba hali haikuwa shwari baada ya mlango wa nyumba ya marehemu kutofunguliwa kwa muda mrefu. Alisema kuwa baada ya kuufungua, walimkuta akiwa amelala sakafuni.

“Amekuwa akiishi peke yake na alikuwa akitegemea biashara yake ya uuzaji kuni. Tulianza kushuku kwamba hali haikuwa shwari baada ya mlango wake kukaa sana bila kufunguliwa. Tulipochunguza vizuri, tuliona shimo kubwa nyuma ya nyumba yake ya mbao. Tungali kufahamu kiini cha mauaji hayo,” akasema Bi Wangari.

Kulingana na chifu wa Kata ya Maina, Joseph Muraya, kuna ishara kwamba mwathiriwa alidhulumiwa kimapenzi kabla ya kuuawa.

“Uchunguzi wa kina wa mwili wake unaonyesha kwamba alidhulumiwa kimapenzi kabla ya kunyongwa,” akasema.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Nyahururu, Bi Julia Irungu alisema maafisa wa upelelezi wameanza uchunguzi kubaini kilichosababisha mauaji hayo.