Habari Mseto

Rais apigwa na butwaa wabunge wake wakikaa ndeee wasijue yanayojiri Serikalini

February 20th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto ameshangazaa kugundua wabunge wa serikali ya Kenya Kwanza hawana ufahamu kuhusu nafasi za kazi ambazo amefaulu kupata katika safari zake za ughaibuni.

Hii ni baada ya wabunge kumuambia Rais kuwa hawajafahamishwa kuwa serikali imepata nafasi za ajira za kuwafaa Wakenya.

Rais alipigwa na butwaa baada ya wajumbe kuweka malilio yao bayana.

Haya yalijiri Jumatatu katika mkutano wa mawaziri na wabunge wa serikali ya Kenya Kwanza walipokutana Naivasha, Kaunti ya Nakuru kutathmini utendakazi wa utawala wao.

“Hakuna mtu ametufahamisha!” mbunge mmoja alimkata kauli Rais alipokuwa anazungumza.

“Nimekuwa nikiongea kuhusu hili katika kila mkutano mfululizo. Sasa wewe unapokaa katika mkutano huu na kusikia Rais akisema kuna kazi ya wauguzi, huwezi kuenda kutafuta habari kuhusu kazi hizi?” Rais aliwauliza Wabunge.

Ilibidi Dkt Ruto awasisitizie wabunge kuwa kuna kazi 2,000 za wauguzi Saudi Arabia baada ya wauguzi 500 pekee kutuma maombi.

Rais alishangaa kuwasikia wabunge wakikosa ufahamu akisema tangazo la kazi hizo lilipeperushwa na vyombo vya habari.

Hata hivyo, Kiongozi wa Taifa aliwaahidi wabunge kuwa atakamilisha kituo cha mawasiliano ili Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira ishirikiane nao kupitisha habari.

Aliweka wazi kuwa serikali ya Ujerumani inahitaji wafanyakazi 250,000 kutoka Kenya.

Serikali inatarajiwa nchi hizi mbili zitatia sahihi mkataba wa ushirikiano ifikapo Juni 2024.