Habari Mseto

Mwanamume afariki katika hali tata Kambi Moto

February 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO katika eneo la Makadara wanachunguza kisa cha kuhuzunisha na kinachoshangaza ambapo mwanamume alifariki katika hali ya kutatanisha.

Akiongea na Taifa Leo mnamo Februari 13, 2024, Kamanda wa Polisi Kaunti ndogo ya Makadara Judith Nyongesa alisema kisa hicho kilitokea mwendo saa tano unusu usiku katika eneo la Kambi Moto lililoko katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba.

Bi Nyongesa alithibitisha kwamba ripoti iliyoandikishwa na mkewe marehemu, Bi Christine Nasimiyu ni kwamba Bi Christine alikuwa amelala wakati wa tukio.

Aliongeza kwamba Bi Christine aliamshwa na kelele iliyokuwa nje na wakati alipoamka na kutoka nje ya nyumba, alipata mwili wa mumewe ukilala chini njiani takriban mita kumi kutoka kwa mlango wa nyumba yao.

“Mjane alikuwa amelala wakati wa tukio. Alisema aliamshwa na kelele kutoka nje na  alipofunga mlango na kutazama, aliona mwili wa mumewe ukilala njiani karibu mita 10 kutoka kwa nyumba yao eneo la Kambi Moto,” Bi Nyongesa akasema.

Vilevile, ripoti za polisi zilionesha kwamba mwili huo haukuwa na alama ya kushambuliwa wala kujeruhiwa.

Awali, wakazi walisambaza habari za tukio hilo wakidai kwamba kuna mwili uliopatikana njiani wa mwanamume aliyedaiwa kushambuliwa kwa kuchomwa kisu nyakati za usiku katika eneo hilo hilo.

“Wakazi wanadai mwanamume alishambuliwa na genge la wahalifu waliomvamia na kumchoma kisu mwanamume mmoja Kambi Moto na mwili kupatikana ukilala njiani na watu wakirauka kwenda kazini mwendo wa saa kumi na moja za asubuhi,” Bi Alice Khalumba akasema.

Kadhalika, Bi Nyongesa alitoa onyo kwa wananchi kwamba ni makosa kusambaza habari sisizo sahihi hasa zinazohusiana na masuala ya kifo.

Pia, ni hatia kwa yeyote kusambaza habari za uwongo na zilizo za kupotosha.

Mwili wa mwanamume huyo ulipelekwa katika mochari ya City kusubiri upasuaji.

Bi Nyongesa alisema kisa hicho kimechukuliwa na polisi na kurekodiwa kama kisa cha Kifo cha Ghafla.