Hofu Mackenzie na wenzake watahepa wakiachiliwa kwa dhamana
MAHAKAMA ya Mombasa imeambiwa kuwa, washukiwa wa mauaji yaliyotokea Shakahola hawana makao yanayofahamika kwa vile wengi wao walikuwa wamehama ili kuishi katika msitu huo ulio Kilifi ambao sasa ni eneo la uhalifu lililofungwa.
Upande wa Mashtaka uliambia mahakama kuwa, kwa msingi huo, mshukiwa mkuu Paul Mackenzie na washukiwa wengine 94 wanaweza kutoroka, kwa hivyo hawafai kuachiliwa kwa dhamana.
Kiongozi wa mashtaka, Bw Victor Simbi, alimwambia Hakimu Mkuu wa Mombasa, Bw Alex Ithuku, iwapo washtakiwa wataachiliwa kwa dhamana, itakuwa vigumu kuwapata na kuwawasilisha mahakamani wanapohitajika.
Mackenzie na washtakiwa wenza walikanusha mashtaka 238 ya mauaji bila kukusudia yanayohusishwa na vifo vya Shakahola.
Kulingana na upande wa mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mazito sana na hivyo wana kila sababu ya kutofika mahakamani iwapo watapewa uhuru.
Upande wa mashtaka ulisema kuwa, kila mshtakiwa alikuwa na ushawishi kwa mashahidi ambao wana uhusiano wa karibu kama vile viongozi wa dini, wazazi na washirika wenzao ambao walishawishi watu kufunga hadi kufa.
“Baadhi ya mashahidi ni watoto wa washtakiwa. Iwapo wataachiliwa na kutangamana na watoto hao, basi kesi ya upande wa mashtaka itavunjika,” alisema Bw Simbi.
Mawakili wa washtakiwa, Mabw Wycliffe Makasembo na Lawrence Obonyo, walipinga vikali ombi la kuwanyima washtakiwa dhamana wakisema kuwa halikuwa na msingi wowote.
Bw Makasembo alisema kuwa ombi la upande wa mashtaka ni la tetesi tupu akisema kuwa hakuna sababu mwafaka zilizotolewa kuwanyima washtakiwa dhamana.
“Kunyimwa dhamana kusitumiwe kama adhabu, washtakiwa lazima wachukuliwe kuwa hawana hatia hadi wanapopatikana na hatia,” alisema Bw Makasembo.
Aliongeza kusema kuwa washtakiwa kuwa na kesi nyingi sio msingi wa kuwanyima dhamana.
Kesi hiyo hapo jana ilisikizwa bila washtakiwa kwa kuwa baadhi yao walishindwa kutembea hadi mahakamani kwa kuwa walikuwa ‘hawana nguvu’ kwa madai ya kususia chakula kwa siku nne. Kesi imepangwa kutajwa Machi 5.
Bw Obonyo ambaye anamwakilisha mke wa Mackenzie aliiambia mahakama kuwa, mshtakiwa alikuwa amejiwasilisha mwenyewe katika mahakama ya Shanzu na kwamba alikuwa ndiye anayemwangalia mtoto wa chini ya miaka sita.
Wakili huyo aliiambia mahakama izingatie utaratibu wa kupeana dhamana na pia katiba na isizingatie matamshi ya umma.