Kaunti zipewe ufadhili wa 47% kwenye marekebisho ya Katiba – Makanisa
Na PIUS MAUNDU
BARAZA la Kitaifa la Makanisa Kenya (NCCK) sasa linashinikiza mageuzi ya Katiba ili kustawisha ukuaji wa kiuchumi kupitia ugatuzi.
“Katiba inapaswa kutathminiwa upya ili kuongeza kiwango cha fedha ambacho kinatengewa kaunti kutoka asilimia 15 hadi 47. Hilo litaongeza kasi ya maendeleo katika kaunti hizo,” akasema Askofu Timothy Ndambuki, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo. Kulingana naye, kuongezwa kwa mgao huo wa fedha pia kutapunguza kiwango cha ufisadi katika kaunti.
Askofu huyo, alitoa kauli hiyo mnamo Jumamosi kwenye hafla ya kuwahamasisha wakazi kuhusu umuhimu wa kutega maji ya mvua katika Shule ya Upili ya Malaa, Kaunti ya Makueni. Askofu huyo, ambaye pia ndiye mkuu wa kanisa na ABC katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini aliandamana na mshirikishi wa baraza hilo katika eneo la mashariki Faith Sibairo.
“Sakata za ufisadi ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika serikali ya kitaifa zinachangiwa na hali kuwa baadhi ya idara zinazotengewa fedha huwa hazizitumii kwani huwa hazina mipango maalum ya maendeleo. Fedha hizo zinapaswa kutengewa serikali za kaunti,” akasema Bw Ndambuki.
Alisema kuwa eneo la Ukambani lilikuwa limebaki nyuma kimaendeleo, ila hali hiyo imebadilika kutokana na uwepo wa ugatuzi.
Miongoni mwa waliohutubu kwenye hafla hiyo ni Gavana Kivutha Kibwana, Naibu Gavana Adelina Mwau, mbunge wa Mbooni Erastus Kivasu na Kiongozi wa Wengi katika kaunti hiyo Kyalo Mumo.
Waliozungumza walisifia mipango ya utegaji maji inayoendelezwa na wakulima binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali ya kaunti hiyo, wakisema kuwa yatabadilisha maisha ya wakazi.
Viongozi waliwahimiza wakazi kutumia kilimo cha maji kuanza miradi itakayoimarisha maisha yao.