Habari Mseto

Polisi watatu mashakani kwa kuitisha Sh200,000 kuwaachilia wauzaji bangi

February 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

MAAFISA watatu wa polisi kutoka Kaunti ya Murang’a wanaendelea kuchunguzwa kwa madai kuwa waliitisha hongo kuwaachilia washukiwa watatu walionaswa na bangi.

Polisi hao wa kiume walipata habari kuwa kulikuwa na wanawake watatu ambao walikuwa wakiuza bangi viungani mwa mji wa Kenol, Murang’a Kusini. Badala ya kufuata sheria na kuwanasa, inadaiwa waliitisha hongo ya Sh200,000 ili kuwaachilia.

Polisi hao walikuwa wakihudumu katika vituo vya polisi vya Kabati na Kenol na mwingine alikuwa wa kupiga doria. Wangefaulu, wangeenda nyumbani na kitita hicho cha pesa.

“Inadaiwa kuwa watatu hao waliwafumania wauzaji bangi wakiwa na bidhaa hiyo kiasi cha kilo 200 katika lokesheni ya Wempa, eneobunge la Maragua na wakaitisha hongo ya Sh200,000,” ilisema ripoti ya polisi.

Washukiwa hao walijaribu na kufanikiwa kutoa Sh120,000 na wakaomba wapewe muda zaidi wa kusaka masalio ya Sh80,000. Polisi hao walichukua pesa hizo na kutwaa bangi wakilalamika.

Wakifanya hivyo, hawakufahamu walikuwa wakiandamwa na wenzao.

Ugomvi ulizuka kati ya maafisa hao, baadhi wakitaka wenzao waachiliwe huku wengine wakitaka wenzao washughulikiwe kama watu walionaswa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kisha washtakiwe kortini.

Naibu Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini alisema kuwa bado hawakuwa wamepata maelezo kuhusu tukio hilo na wameanzisha uchunguzi dhidi ya polisi hao.